HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

July 23, 2026

CRDB Yazindua Msimu Mpya wa Zogo Mchongo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


BENKI ya CRDB imezindua msimu wa nne wa kipindi cha Zogo Mchongo kinacholenga kuimarisha elimu ya fedha kwa Watanzania kupitia televisheni na majukwaa ya kidijitali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa matumizi salama ya huduma za kifedha na kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.


Akizindua msimu huo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda, alisema mpango huo unaunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi wengi kwa njia rahisi, za kisasa na zenye kuendana na maendeleo ya teknolojia.


Makonda alisema matumizi ya wasanii na majukwaa ya kidijitali katika utoaji wa elimu ya fedha yatawawezesha wananchi kujifunza kuhusu uwekezaji, biashara, matumizi sahihi ya mikopo pamoja na kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kuboresha maisha yao.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo imeendelea kutekeleza falsafa yake ya Zaidi ya Benki kwa kuwekeza katika elimu ya fedha kwa jamii.



Alisema maendeleo ya teknolojia na matumizi ya akili unde yanahitaji wananchi kuwa na maarifa ya kutosha yatakayowawezesha kutumia huduma za kifedha kwa usalama, kuongeza ufanisi wa shughuli zao za kiuchumi na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.


Dk. Nsekela alibainisha kuwa kupitia msimu mpya wa Zogo Mchongo, CRDB itaendelea kuwafikia wananchi kwa maudhui yanayohusu uwekezaji, biashara, akiba, mikopo na matumizi salama ya huduma za kifedha kwa njia za kidijitali.


Alisisitiza kuwa jamii yenye maarifa ya kifedha ndiyo msingi wa kujenga uchumi jumuishi, kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages