HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 08, 2015

TAARIFA YA HALI YA MWENENDO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA NA MVUA ZA MSIMU WA VULI 2015

UTANGULIZI 
 Taarifa hii inatoa tathmini ya mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na msimu wa mvua za vuli kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka pamoja na mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu moja wa mvua kwa mwaka katika kipindi cha Novemba-Desemba 2015. 

MIFUMO YA HALI YA HEWA
Kuendelea kuongezeka kwa joto katika maeneo ya Bahari ya Pasifiki kunaonesha kuimarika kwa El-Nino katika Bahari ya Pasifiki kama ilivyoelezwa katika taarifa ya Mamlaka iliyotolewa mapema mwezi Septemba, 2015. 

Hata hivyo, mifumo mingine ya hali ya hewa ikiwemo mwitikio wa mfumo ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi imekuwa na mchango hasi kinyume na ilivyotarajiwa katika mwenendo wa mvua za Vuli nchini katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2015 na kusababisha vipindi virefu vya upungufu wa mvua katika Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam. Hata hivyo mifumo ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa pwani ya Angola katika Bahari ya Atlantiki imenza na inaendelea kuimarika. 

Kuimarika kwa mifumo hii kunatarajiwa kusababisha kunyesha kwa mvua katika maeneo mengi kama zilivyotabiriwa katika kipindi cha mwezi Novemba-Disemba 2015. Kwa upande mwingine, mpaka sasa baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Ukanda wa Ziwa Viktoria yameendelea kupata mvua za wastani katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2015.

 MVUA KWA MWEZI NOVEMBA HADI DISEMBA 2015 
Maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria, Kanda ya Magharibi na Nyanda za juu kaskazini Mashariki yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani katika kipindi cha mwezi Novemba hadi Disemba 2015, pamoja na vipindi vifupi vya mvua kubwa. 

Kwa ujumla mwelekeo wa mvua bado ni kama ulivyotolewa mapema tarehe 2 Septemba 2015. Maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka Mikoa ya Dodoma, Singinda, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa, Njombe, Tabora, Kigoma Rukwa na Katavi mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili na ya nne ya mwezi Novemba, 2015. Ambapo mvua hizo zimeanza kujiimarisha katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine mwezi huu wa Novemba 2015. Hata hivyo, Wilaya za Kondoa, Kongwa na Singida Vijijini katika mikoa ya Dodoma na Singida zinatarajiwa pia kupata vipindi vya mvua mapema mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2015. 

USHAURI 
Mamlaka ya Hali ya Hewa inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika katika kutekeleza mipango inayoweza kuathiriwa na mwelekeo wa hali ya hewa iliyotabiriwa.Tahadhari zilizotolewa na Mamlaka sambamba na taarifa hii ya mrejeo ziendelee kuzingatiwa . 

VYOMBO VYA HABARI 
Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kutumia wataalam wa sekta husika katika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kwa jamii. Aidha, jamii nayo inashauriwa kufuatilia na kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa na mirejeo yake. 

Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi viashiria vya mvua katika kipindi cha msimu(miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. 

Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na wa mwezi kama zinavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania. Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini. 

Dkt. Ladislaus B. Chang’a KAIMU MKURUGENZI MKUU

No comments:

Post a Comment

Pages