HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 22, 2015

Rebecca Malope kutua Desemba 24

MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili Afrika, Rebecca Malope (pichani) anatarajia kuwasili nchini Desemba 24 tayari kuja kuungana na waimbaji wengine wa ndani na nje kupamba Tamasha la Pasaka litakalofanyika Desemba 25 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijiji Dar es Salaam.

Akithibitisha hilo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama, Malope atawasili katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere majira ya saa tisa alasili.

Msama alisema ingawa Malope atawasili kesho, wasaidizi wake watatua nchini leo kwa ajili ya kufanya maandalizi ya awali kuelekea tamasha hilo ambalo tayari limekuwa gumzo kubwa kwa wapendwa, wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili.

Alisema, mwimbaji Faustine Munishi kutoka Kenya, aliwasili tangu jana usiku akitokea huku mwimbaji Sarah K pia kutoka nchini Kenya, naye akitarajia kuwasili kesho majira ya saa 10 jioni.


Msama mwasisi wa matamasha ya muziki wa injili tangu mwaka 2000, alisema Solomon Mukubwa anatarajia kutua nchini Ijumaa asubuhi na kueelekea moja kwa moja ukumbini kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kwa Watanzania.

Aidha, Msama ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo ili kurudisha shukrani kwa Mungu baada uchaguzi Mkuu uliofanyika kwa amani.

“Nawasihi wapendwa wa Mungu, wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili, wajitokeze kwa wingi katika Ukumbi wa Diamond Jubilee tuburudike pamoja na kumrudishia Mungu shukrani baada ya kuvuka salama katika Uuchaguzi Mkuu uliofanyika kwa amani na utulivu,” alisema Msama.

Kwa upande wa viingilio katika tamasha hilo, ni shilingi 50,000 kwa Viti maalum, VIP shilingi 10,000, shilingi 5000 viti vya kawaida na shilingi 2000 kwa watoto.

“Viingilio tulivyopanga vitasaidia wenye uhitaji maalum kama yatima, walemavu, wajane na wengineo ambao wanahitaji msaada,” alisema Msama.

Waimbaji wengine katika tamasha hilo ni Rose Muhando, Upendo Nkone, Jesca Honore, Christopher Mwahangila, Joshua Mlelwa, Martha Mwaipaja, Christina Shusho, Sifael Mwabuka, Kwaya ya KKKT  Yombo na Kwaya ya Wakorintho wapili ambayo itazindua albamu yake ya Mchepuko sio dili.

Waimbaji wa nje ni pamoja na Rebecca Malope (Afrika Kusini), Sarah K, Solomon Mukubwa na Faustin Munishi ‘Malebo’  (Wote kutoka Kenya).

Msama alisema mgeni rasmi katika tamasha hilo ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.

No comments:

Post a Comment

Pages