Wakili
wa Nemc, Manchele Suguta (kushoto) akizungumza na mawakili wa walalamikaji,
George Mwalali (kulia) na Abubakar Salim mara baada Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, kuweka zuio
la kusitisha ubomoaji wa nyumba zaidi ya 681 za wakazi wa mabondeni jijini Dar
es Salaam. (Picha na Francis Dande)
Wakati shauri lao likiendelea wakazi wa mabondeni wakiwa wametulia kusubiri maamuzi ya mahakama.
Magari ya Polisi yakiwa yameimarisha ulinzi.
Wakati shauri lao likiendelea wakazi wa mabondeni wakiwa wametulia kusubiri maamuzi ya mahakama.
Magari ya Polisi yakiwa yameimarisha ulinzi.
Polisi wakiwa wameweka ulinzi mkali nje ya mahakama.
Wakili
wa Nemc, Manchele Heche akizungumza na waandishi wa habari.
Wakili wa wakazi wa mabondeni, Abubakar Salim akizungumza na waandishi wa habari.
Wakazi wa mabondeni waliofungua kesi ya kupinga kubomolewa nyumba zao wakimsikiliza mbunge wao, Maulid Mtulia CUF)
Tulieni tulieni...........
Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF), akizungumza na wakazi wa mabondeni mara baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutoa uamuzi wa kuweka zuio la ubomoaji wa nyumba 681 za wakazi wa mabondeni.
Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF), akiwapungia mkono wananchi waliokuwa wamefurika nje ya mahakama.
DAR ES SALAAM, Tanzania
Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi leo Januari 5 imeweka zuio la kusitisha ubomoaji
wa nyumba 681 za wakazi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es
Salaam.
Hata hivyo kabla
ya mahakama kutoa amri hiyo, kazi ya ubomoaji wa nyumba za wananchi hao ilikuwa
ikiendelea hata kwa walalamikaji 681 ambao walikuwa wakisubiri amri ya mahakama.
Hali hiyo
imetafsiriwa kuwa ni ukatili na unyama wa hali ya juu wanaofanyiwa wakazi wa Jiji
la Dar es Salaam, kwani watekelezaji wa kazi hiyo walipaswa kusubiri uamuzi wa mahakama.
Baada ya uamuzi wa mahakama kuweka zuio, tingatinga liliendelea
kubomoa nyumba za wananchi hao zaidi ya 100 katika
bonde la Mkwajuni, Kata ya Hananasif huku nyumba zaidi ya 5,000 zikiwekwa
alama ya X tayari kwa kuvunjwa.
Uamuzi wa shauri
hilo umetolewa siku moja baada ya Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) na
walalamikaji wengine wanane, wakiwakilisha wenzao 681, kufungua kesi ya kupinga
ubomolewaji wa nyumba hizo.
Katika kesi hiyo
namba 822 iliyofunguliwa dhidi ya Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Taifa la
Usimamizi wa Mazingira (Nemc) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), chini ya
Jaji Penterine Kente, juzi ilianza kusikilizwa lakini kutokana na mvutano mkali
wa kisheria kutoka pande mbili baina ya serikali na walalamikaji, iliahirishwa
hadi jana kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
Pamoja na Mtulia,
wengine walioshiriki kufungua kesi hiyo na kuwawakilisha wenzao 681 ni Alli
Kondo, Agness Machalila, Sanura Abeid, Sultan Ally, Mussa Hassan, Godwin
Cuthbert na Rene Duma.
Akitoa uamuzi wa
kubomolewa au kutokubomolewa kwa nyumba hizo jana saa nane mchana badala ya
muda uliotarajiwa wa saa tano asubuhi, Jaji Kente alisema licha ya kuibuka hoja
mbalimbali katika usikilizwaji wa awali wa shauri hilo, baadhi hazikuwa za
msingi.
Alisema hoja
kubwa ambayo inasubiriwa na watu ni ombi la kuzuia ubomoaji wa nyumba 681 ambao
umewakilishwa na watu wanane, huku swali kubwa ni kwamba mahakama itaweza kutoa
zuio la ubomoaji au la?
Jaji Kente
alisema kuwa suala hilo limekuwa na ugumu kutokana na ukubwa wake, lakini bado
anayo ya kusema, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali zina nia
njema, pia anakubaliana na kushawishika kwamba hatua zote zinafuata sheria.
Alisema kwa kuwa
mchakato huo umekuwa na athari kubwa kwa wanaobomolewa, basi kuingilia kati kwa
mahakama ni muhimu kwa sababu inawalinda watu hao.
“Sina ushahidi
wa serikali wala walalamikaji kutokana na kukosa ushahidi wa kina kwa kuwa kesi
haijaanza kusikilizwa, pia hata upande wa walalamikaji haujaleta majina yote,” alisema.
Licha ya hayo,
Jaji Kente alisema ni vema ifikie wakati watu wakubaliane kwamba katika shauri
hilo kuna watu walioguswa na hatua hizo za serikali.
“Kutokana na
hayo, mahakama imesitisha kubomolewa nyumba za waombaji hao hadi hapo shauri la
msingi lililofunguliwa kupinga ubomolewaji huo litakaposikilizwa na kutolewa
uamuzi,” alisema.
Hata hivyo, Jaji
Kente alisema ili kuondoa shaka dhidi ya zuio hilo, serikali inaweza kuendelea
na mchakato wa kuweka alama na kuvunja nyumba ambazo hazitambuliki mahakamani.
“Zuio hili linawahusu
wale waombaji 681 waliofikisha maombi yao mahakamani na si vinginevyo. Kwa wale
wasiohusika serikali inaweza kuendelea na mchakato wake kama kawaida,” alisema.
Hata hivyo, Jaji
Kente aliwataka baadhi ya waombaji hao 681 kuhakikisha wanawasilisha orodha ya
majina na anuani zao kwa kuwa awali yalikuwa ya watu wanane tu.
Baada ya kusema
hayo, Jaji Kente alisema kuwa licha ya kutolewa kwa zuio hilo lakini kuna kesi
ya msingi ambayo itaendelea kusikilizwa Januari 11, mwaka huu.
Wakili wa Nemc,
Manchare Heche, alisema licha ya kutolewa kwa uamuzi huo, mchakato huo
utaendelea kama ilivyopangwa ili kuhakikisha taratibu zinafuatwa.
Alisema kuwa kutokana
na uamuzi huo na hadi kesi hiyo itakapoisha ni vema wananchi hao wazidi
kujiweka katika hali ya maandalizi ya kuhama kabla ya kubomolewa.
“Huu mchakato
unawalinda wao, ndiyo maana tunawaondoa mabondeni, lakini tutaendelea kubomoa
zile nyumba zote ambazo hazikuhusika katika ufunguaji wa kesi hii kama mahakama
ilivyosema,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali
inasisitiza kwamba watu wa mabondeni waondoke kwa hiari yao katika maeneo hayo,
licha ya kuwa kesi inaendelea.
Nje ya mahakama
hiyo iliyopo maeneo ya Sokoine idadi kubwa ya wananchi ilijitokeza kwa ajili ya
kushuhudia uamuzi wa kesi hiyo.
Mamia ya watu
walianza kujikusanya kwa makundi kuanzia saa mbili asubuhi, ambapo wengine
walikaa pembezoni mwa barabara na kusababisha magari kupita kwa shida.
Wakati idadi
hiyo ikijitokeza kwa ajili ya kusikia uamuzi huo uliotarajiwa kutolewa saa tano
asubuhi, lakini baadaye uliahirishwa hadi saa nane na Jeshi la Polisi
liliongeza ulinzi katika maeneo hayo.
Ilipotimu saa tano
asubuhi idadi kubwa ya wananchi walikuwa na shauku ya kujua nini kinaendelea,
lakini walikatishwa tamaa baada ya Mbunge Mtulia kuwatangazia muda wa kesi hiyo
kutolewa uamuzi umesogezwa mbele.
Kutokana na
kauli hiyo, baadhi ya wananchi walisikika wakiwahamasisha wenzao kwamba hakuna
kuondoka eneo hilo hadi wajue hatima yao, ikiwezekana wakanunue vyakula walie
hapo hapo.
“Hakuna kuondoka
mtu hapo, nunua muhogo hapo kuleni hapa hadi kieleweka,” alisikika mmoja wa
wananchi hao akisema.
No comments:
Post a Comment