Tamasha hilo ambalo
limekuwa likisambaa katika mikoa mbalimbali baada ya uzinduzi wake kufanyika
jijini Dar es Salaam limekuwa likipambwa na waimbaji mahiri wa kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuutukuza
ufalme wa Mungu na malengo mengine kibao.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la
Pasaka, Alex Msama (pichani), anasema tayari ameanza pokea maombi kutoka kwa mashabiki wa muziki
wa injili wa mkoa wa Morogoro, Mwanza, Mbeya, Dodoma wakitaka tamasha hilo lianzie
kwao badala ya Dar es Salaam.
“Ingawa ni mapema mno,
Kamati yangu inatarajia kufuatilia taratibu za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata)
ambazo ni pamoja na kibali cha kufanikisha Tamasha hilo linaloshirikisha
waimbaji wa ndani na nje ya Tanzania,” alisema Msama.
Kwa upande wake Salum
Ismail Hamad wa jijini Dar es Salaam, mmoja wa wadau wa Tamasha hilo amewasihi
waratibu kutopeleka kwingine uzinduzi wake, badala yake ubaki katika jiji hilo kutokana
na wingi wa mashabiki kabla ya kuhamia mikoani.
Naye Rukia Joseph wa
Kimara, alisema Tamasha hilo lenye historia inayoanzia mwaka 2000, wanapaswa kuendeleza
utaratibu wa kuanzia katika jiji la Dar es Salaam kabla ya kugeukia mikoani.
Aidha, Michael Deogratius
alisema angependa kuona Tamasha hilo la Pasaka lihamie mikoani badala ya
kuanzia jijini Dar es Salaam kila mwaka ili kuleta usawa kwasababu huko nako
kumekuwa na mwitikio mkubwa wa muziki wa injili.
Akifafanua kuhusu maoni
yao ya wadau, Msama alisema ni mawazo mazuri kuyapata kipindi hiki ambapo
maandalizi rasmi bado hayajaanza kwani kunawapa picha ya kitu gani wapenzi na
mashabiki wanataka na wao wafanye nini kulingana na uwezo wao kifedha.
Tamasha la Pasaka ndilo
tukio kongwe zaidi la muziki wa injili ambalo limekuwa likifanyika wakati wa
sikukuu ya Pasaka tangu mwaka 2000 kwa lengo la kumtukuza Mungu na malengo
mengine yakiwamo kupata fedha za kusaidia makundi maalumu katika jamii.
No comments:
Post a Comment