HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 21, 2016

‘Kekundu’ ndani ya Tamasha la Pasaka .Kiingilio chapangwa buku tano

Mwenyekiti wa Tamasha la Pasaka, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika Machi 26 mkoani Geita. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi, Khamis Pembe.  (Picha na Francis Dande)
 Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha la Pasaka, Khamis Pembe akizungumzia jinsi walivyoipanga katika kuhakikisha usalama unakuwa wa uhakika wakati wa tamasha hilio.

Na Mwandishi Wetu


KWAYA ya AICC Shinyanga maarufu kwa jina la ‘Kekundu,’ nayo imeteuliwa kutumbuiza Tamasha la Pasaka litakalofanyika katika mikoa ya Mwanza, Geita na Wilaya ya Kahama kuanzia Machi 26 katika kusindikiza tukio la kukumbuka ufufuko wa Yesu Kristo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Alex Msama, alisema anashukuru kitendo cha kwaya hiyo maarufu kukubali kuungana na nyingine kulipa uzito tamasha hilo lenye malengo kibao tangu kuanzishwa kwake.

Msama alisema mbali ya kuadhimisha kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo, pia sehemu ya mapato ya milangoni yamekuwa yakisaidia makundi maalumu kama yatima, walemavu na wajane na mwaka huu wamepanga kutumia sehemu ya mapato hayo kununua baiskeli 100 ambazo zitagawiwa katika mikoa mbalimbali.

Msama pia ametumia fursa hiyo kuwasihi wadau, wapenzi na mashabiki wa muziki wa Injili kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo kote litakakofanyika kwani kujitokeza kwao ndiyo mafanikio ya malengo ya Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa upande wa burudani, mwimbaji Joshua Mlelwa, ameongezwa katika orodha ndefu ya waimbaji watakaohudumu katika tamasha hilo kutoka ndani na nje ya Tanzania.

“Mbali ya tamasha hili kushirikisha waimbaji mahiri wa ndani na nje ambao kila mmoja atawafurahia, pia tumetoa upendeleo kwa waimbaji chipukizi kwa lengo la kuwapa fursa ya kuchota uzoefu ili kuwa waimbaji bora wa siku zijazo,” alisema.

Msama ameongeza kwamba kiingilio la tamasha hilo kote litakakofanyika ni shingili 5,000 kwa watu wakubwa na shilingi 2,000 kwa  watoto na kutoa wito kwa wadau kujitokeza kwa wingi siku hiyo, kwani maandalizi yamekamilika kwa asilimia 90.



No comments:

Post a Comment

Pages