NA MWANDISHI WETU
WADAU wa sekta ya Usafiri wa anga nchini wamekutana
katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA)
yaliyopo Banana-Ukonga, jijini Dar es Salaam kujadili rasimu ya mpango kamambe
wa usafiri wa anga.
Katika Warsha hiyo ya siku moja iliyowakutanisha
wadau kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, mashirika
yanayotoa huduma za usafiri wa anga, Mamlaka ya Viwaja vya Ndege na mwenyeji
Mamlaka ya Usafiri wa Anga, ilifunguliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Dk. Leonard Chamuriho.
Lengo la warsha hiyo ni kupata maoni ya
wadau kuhusu rasimu hiyo ya mpango kamambe wa sekta ya usafiri wa anga ambayo imetayarishwa na kampuni ya LEAPP ya
Australia chini ya udhamini wa Benki ya Dunia.
Kampuni hiyo ilianza kuanda rasimu hiyo
mwaka 2015 kazi ambayo imefanyika kwa miezi 12.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo,
Dk. Chamuhiro alisema lengo la serikali ni kuwezesha Tanzania kutoa huduma
za usafiri wa anga kwa viwango na taratibu zinazokubaliwa na Shirika la
Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).
Alisema malengo mengine ni kuweka
mazingira mazuri yatakayoruhusu ushindani wa kibiashara katika sekta hii
na kuongeza kua, sekta ya usafiri wa anga imekuwa ikikua siku hadi siku
kutokana na juhudi mbalimbali.
Dk. Chamuhiro alisema, takwimu zinaonesha
safari za ndege kwa sasa zimeongezeka
kwa asilimia 8 kwa mwaka 2015 ikilinganishwa na zile zilizofanyika mwaka
2014.
Aidha, idadi ya abiria imekuwa ikikua kwa
kiwago cha asilimia 1.5 hadi 2 kwa mwaka na lengo la warsha hiyo, ni kupata
maoni ya wadau kuhusu rasimu hiyo ya mpango kamambe wa sekta ya usafiri wa anga
nchini iliyotayarishwa na kampuni ya LEAPP ya Australia chini ya udhamini
wa Benki ya Dunia.
No comments:
Post a Comment