Zahanati isiyotumika kwa miaka 12
Na Bryceson Mathias,
Mwalazi Nyandira
WAKAZI 1,500 wa Kijiji cha
Mwalazi, Kata ya Nyandira, Tarafa ya Mgeta, wako hatarini kuathirika na
Magonjwa ya Mlipuko, Malaria, Vifo vya Watoto na Wajawazito, kutokana na Zahanati
yao ya Kitongoji cha Mbigila kutofanya kazi kwa miaka 12.
Hayo yamesemwa na Wajawazito
waliodai, wakiwa na Magonjwa ya Mlipuko, Uzazi na Malaria, hubebwa na Machela, Vitanda,
Mizeganzega hadi Mgeta Kilomita Tano na Kibuko Kilomita Tatu kwa kupanda Mlima,
huku maisha yao yakiwekwa rehani.
Wakizungumza na Wandishi siku
ya akina Mama duniani jana, Wajawazito
walioomba wasitajwe wameilaumu Serikali Kuu na watendaji wakidai, Zahanati hiyo
isipofunguliwa watakufa kwa Magonjwa hayo na Uzazi ikiwemo Degedege kwa watoto
wadogo.
“Tukipata dharura za Uzazi
usiku, tunakuwa hatarini hasa tunapobebwa na Machela, Vitanda au Mizeganzega,
na mara kadhaa tunajifungulia njiani kutokana na umbali na ubovu wa miundo
mbinu, hali ambayo ni hatari kiafya wanapotuhudumia.
“Adha hiyo pia inawasibu watoto
wadogo hadi miaka mitano, wanaopata magonjwa ya kitoto likiwemo degedege na
Magonjwa ya Kuhara! Na kijiji chetu cha Mwalazi, kinaongoza kwa Vifo kutokana
na dharura hizo”.alisema mama mmoja mjamzito!
Kaimu Mganga Mkuu wa
Wilaya, Dkt. Omari Mbena, alipoulizwa kwa njia ya simu ya kiganjani hakuwa na
Majibu, na alipoambiwa anazungumza na mwandishi alikwepa maswali akiuliza eneo
walipo wandishi! Na alipoandikiwa Ujumbe mfupi alidai,
“Ndugu yangu ungefika
ofisini ili upate maelezo kamili ya zahanati hiyo maana naweza kukujibu
tofauti”.alijibu Dkt. Mbena, huku wandishi wakihoji, kwa nini anataka waende ofisini
badala ya eneo la tukio?
Hata hivyo alitafutwa
Diwani wa Kata ya Nyandira, Peter Zengwe, na kumbanwa aeleze kinachokwamisha
kufunguliwa kwa zahanati hiyo ili iokoe Maisha ya Wananchi, Watoto na Nguvu
kazi ya Taifa, ambapo alikiri malalamiko ya wakazi ni ya kweli na kudai,
“Zahanati hii ipo tangu
enzi za Mkuu wa Wilaya, Sarah Linuma, imegharimu Mil. 26/- hadi sasa, ila kuna Siasa
chafu zinafanywa isifunguliwe, ingawa imekamilika na Wananchi, Wajawazito na Watoto,
wanaendelea kuteseka kwa kubebwa Machela na Mizeganzega, huku maisha yao yakiwa
hatarini”.alisema Zengwe!
No comments:
Post a Comment