WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa, Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa
katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa ambalo
litatoa fursa kwa wilaya nyingine kama Kilwa, Nachingwea na Liwale
kufuata dawa katika duka hilo.
Ujenzi wa duka hilo la dawa ndani ya wilaya ya
Ruangwa umefadhiliwa na Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) na unakadiriwa kugharimu sh milioni 55 mpaka
kukamilika kwake ambapo kutasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa hospitalini
hapo na katika hospitali zingine zilizoko katika wilaya za jirani.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema mbali na ujenzi wa
duka la dawa pia hospitali hiyo inatarajiwa kujengewa uzio ili kuepusha vitendo
vya uhalifu vinavyoweza kutokea kutokana na hospitali hiyo kukosa uzio.
Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo wakati
akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuweka
jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa katika Hospitali hiyo.
“Nataka hapa ndio iwe bohari ya dawa, watu kutoka
Kilwa, Nachingwea na Liwale wawe wanafuata dawa na vifaa tiba katika duka la
dawa lililoko ndani ya Hospitali ya wilaya ya Ruangwa, pia kujengwa kwa duka hili
kutasaidia kumaliza tatizo la upungufu wa dawa,” amesema.
Amesema mkakati uliokuwepo ni kuhakikisha vifaa tiba
na dawa vinapatikana hospitalini hapo
ili kuwawezesha wagonjwa kupata huduma bora. “Kinachomuuma ni kuona akinamama,
akinababa, vijana na wazee wangu wanakwenda hospitali na kuambiwa vipimo
hakuna, hivyo nitahakikisha ifaa tiba vyote vinapatikana,”.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa HHalmashauri ya
wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo amemshukuru Waziri Mkuu kwa juhudi
mbalimbali anazozifanya ikiwemo kutafuta wafadhili mbalimbali wanaoendelea
kusaidia utoaji wa huduma za afya hospitalini hapa.
“Mpaka sasa kuna mradi wa ujenzi wa uzio wa
hospitali ya wilaya, ujenzi wa duka la dawa, ukarabati wa majengo na upanuzi wa
hospitali na tunamuomba aendelee kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kutatua
changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali yetu ya
wilaya,” amesema.
Dk. Simeo ameongeza kuwa kwa kupitia Waziri Mkuu,
Majaliwa wameweza kupata vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi y ash.
Milioni 100 kutoka umoja wa kampuni unaotengeneza vinywaji baridi nchini ambavyo jana walikabidhiwa na
Meneja wa MSD, kanda ya Mtwara, Helman Mng’ong’o.
Amesema licha ya kupata vifaa hivyo, pia walipokea
vifaa tiba kutoka shirika la VSO vyenye thamani ya sh. milioni 32 ambavyo
vitatumika katika kusaidia watoto waliozaliwa kabla umri haujatimia.
Dk. Simeo alitaja vifaa tiba hivyo kuwa ni ni
mashine ya kusaidia kupumua, mashine ya kusaidia kuhifadhi joto la mototo,
mashine nyingine ni za kusafishia watoto waliopaliwa na mashine ya kusaidia
kujua kiwango cha hewa ya oxygen ndani ya mishipa ya damu ya watoto hao.
Imetolewa na Ofisi ya Waziti Mkuu
No comments:
Post a Comment