WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa, Kassim Majaliwa ameipongeza
timu ya mpira wa miguu ya Namungo FC na kuikabidhi zawadi ya sh. milioni tano
baada ya kuibuka mabingwa wa ligi daraja la tatu mkoa wa Lindi.
Ubingwa huo wa mkoa ulionyakuliwa na timu ya wilaya
ya Ruangwa, umeiwezesha kupanda daraja la pili taifa, hivyo kupata tiketi ya
kushiriki mashindano ya ligi daraja la
pili mechi zitakazochezwa nyumbani na ugenini.
Timu hiyo iliyoanzishwa na wafanyakazi wa mgodi wa
Green Ganet uliopo Namungo, kijiji cha Chingumbwa wilayani Ruangwa mwaka huu imekuwa mabingwa wa ligi daraja la
tatu mkoa wa Lindi hivyo kupata tiketi ya kucheza ligi daraja la pili ngazi ya
taifa.
Akipokea kombe hilo jana Waziri Mkuu, Majaliwa amesema
amefurahishwa na ubingwa huo, ambapo amewataka wadau wa soka wilayani hapa
kuiunga mkono timu hiyo na kuhakikisha inapanda daraja na kucheza ligu kuu ya
Tanzania bara.
Pia amesema atafanya mazungumzo na halmashauri kuona
kama wanaeneo kwa ajili ya kujenga kiwanja cha mpira wa miguu na
litakapopatikana wananchi wanaweza kuanza kujenga mabanda ya biashara kuzunguka
kiwanja hicho na kisha kutafuta mfadhili kwa ajili ya ujenzi wa eneo la
kuchezea.
Kwa upande wake Shanel Nchimbi ambaye ni mmoja wa
viongozi wa timu hiyo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa kuisaidia timu hiyo
katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya ukosefu wa
kiwanja, vifaa vya michezo na vya huduma ya kwanza, usafiri na daktari.
Nchimbi amesema changamoto ya ukosefu wa uwanja
ilisababisha kuutumia uwanja wa michezo wa Sokoine wa wilaya ya Nachingwea kuwa
wa nyumbani hivyo kusababisha timu hiyo kutumia gharama kubwa kufika eneo la
michezo.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
No comments:
Post a Comment