WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) , anafanya uhakiki wa madeni yanayodaiwa serikali na watumishi
na kubaini madudu.
Amesema madai mengine yameonyesha mashaka ambapo
amewataka wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wakuu wa ndani kujiridhisha ukweli
wa madai hayo kabla ya kuyafikisha serikalini kwa ajili ya malipo.
“Madai mengine yanatia mashaka, sisi hatuhitaji
kuletewa madeni ya hovyo hovyo ni vema Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi
wa ndani wakajiridhisha kabla kuyapeleka serikalini kwa ajili ya malipo.
Madeni
mengine ya ajabu, mfano unakuta mtumishi mmoja anaidai serikali sh. milioni
30, jambo ambalo ni gumu hata kama
alihamishwa haiwezekani kufikia kiwango hicho, pia kuna baadhi ya majina
yamejirudia mara nne,” amesema.
Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo wakati
akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa alipotembelea
Hospitali hiyo wakati akiwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukabidhi msaada
wa vifaa tiba alivyovitoa kwa ajili ya hospitali hiyo.
Amesema kuwa serikali italipa madeni yote inayodaiwa
baada ya kumaliza kuyafanyia uhakiki, hivyo aliwaomba watumishi kuwa na subira
wakati serikali ikiendelea zoezi la kuyahakiki ili kuweza kulipa deni sahihi
inalodaiwa.
Awali akisoma taarifa ya Idara ya afya kwa Waziri
Mkuu, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo amesema
idara ya afya inakabiliwa na madeni ya watumishi ambayo ni sh. milioni
109,662,483.
Amesema madeni hayo yametokana na likizo, matibabu,
uhamisho wa ndani na nje ya wilaya, gharama za mizigo kwa watumishi waliostaafu,
ambapo halmashauri imejipangia utaratibu
wa kulipa madeni hayo pindi inapotokea fedha kutoka serikali kuu.
Hata hivyo kasi ya mtiririko wa fedha ni ndogo
ukilinganisha na mahitaji halisi ya maslahi ya watumishi ambapo Halmashauri
inawapongeza na kuwapongeza watumishi wa Idara ya afya kwa kuendelea kuwa
wavumilivu na kuwahudumia wananchi.
Dk. Simeo amesema halmashauri inawapongeza Rais Dk.
John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuongeza
mapato nchini, ambapo wana matumaini kuwa watumishi wataboreshewa maslahi na
stahiki zao ili kuchochea motisha kiutendaji.
Katika hatua nyingine Dk. Simeo alizungumzia
upatikanaji wa dawa, alisema ambao
umeongezeka kutoka asilimia 30 mwaka jana na kufikia asilimia 80 mwaka
huu dawa muhimu katika vituo vyote vya kutolea huduma ambavyo viko 32.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
No comments:
Post a Comment