HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 12, 2016

Mohammed Aboud Mohammed akutana na Viongozi wa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya ofisi yake

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed (wa kwanza kutoka kulia) akiwa katika kikao cha kwanza na Viongozi wa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Ofisi hiyo mara baada ya kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuiongoza Wizara hiyo.
 Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim akielezea faraja kwa niaba ya watendaji wa ofisi hiyo wakati viongozi wa Taasisi za Ofisi hiyo walipokutana kwa mara ya kwanza na Waziri wao Mh. Mohammed Aboud Mohammed ofisini vuga Mjini Zanzibar.
Waziri Aboud akiwaagiza wasaidizi wake kuwasimamia vyema watendaji wao katia kutekeleza majukumu yao yanayotarajiwa kuongezeka kutokana na kazi ya utendaji wa Serikali wa kipindi cha Pili cha Awamu ya Saba. (Picha na – OMPR – ZNZ).

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed alisema ni vyema kwa Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo wakajenga tabia ya kukubali kukosolewa na wafanyakazi walio chini yao zinapotokea hitilafu za kiutendaji wakati wanapotekeleza majukumu yao ya  kazi.

Mh. Aboud alisema hayo katika kikao cha kwanza alipokutana na Viongozi wa Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Ofisi hiyo mara baada ya kuteuliwa tena na Rais wa Zanzibar kushika wadhifa wa kuiongoza Wizara hiyo Kikao kilichofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema Wananchi walio wengi wameanza kujenga matumaini yanayotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa kipindi cha Pili cha Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dr. Ali Mohammed Shein.

Mh. Aboud alieleza kwamba Miaka mitano ijayo itakuwa ya kasi katika utendaji wa Serikali kuu iliyojikita zaidi kuimarisha uchumi na kusimamia Maendeleo kwa kutegemea rasilmali  na vianzio vyake vya mapato.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea matumaini yake kutokana na umakini wa Viongozi walioanza kukabidhiwa majukumu ya kusimamia Taasisi za Umma katika maeneo mbali mbali.

Akizungumzia suala la udhibiti na matumizi sahihi ya fedha pamoja na Vifaa vya Serikali Mh. Aboud aliwakumbusha Viongozi wa Taasisi hizo kuhakikisha kwamba suala hilo wanalisimamia kwa nguvu zao zote kwa kuzingatia  taratibu na kanuni za kazi.

Alisema udhibiti na usimamizi wa matumizi sahihi ya fedha za Serikali ni kitu cha msingi kinachopaswa kushirikisha watendaji na viongozi wa ngazi zote za Taasisi na mashirika ya Umma.

Kuhusu mvua za masika zinazoendelea kunyesha sehemu mbali mbali hapa Nchini Waziri Aboud aliwaagiza Viongozi na Watendaji wa Kamisheni ya Maafa Zanzibar iliyo chini ya Ofisi hiyo kuendelea kutoa tahadhari kwa umma ili kusaidia kupunguza hitilafu zinazoweza kusababisha athari kutokana na mvua hizo.

Alisema athari za maafa zinazotokana na mvua hizo bado zipo ikiwemo uharibifu wa nyumba zilizojengwa mabondeni na vianzio vya maji sambamba na kuendelea kwa maradhi ya maambukizo mambo ambayo viongozi na Wananchi wote wanapaswa kushirikiana katika kukabiliana nayo.

Mapema Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim alisema kwamba watendaji wa Ofisi hiyo wamepata faraja kubwa kutokana na imani ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Moh’d Shein kwa kumteuwa tena Mh. Aboud kushika wadhifa huo.

Nd. Ahmad alisema watendaji wanaamini kwamba kasi ya utendaji kwa Taasisi na mashirikia yaliyo chini ya Ofisi hiyo itaongezeka kutokana na uhusiano na maingiliano ya muda wa miaka mitanoyaliyopo kati ya Kiongozi huyo na watendaji hao.

No comments:

Post a Comment

Pages