WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema vijiji 42 vya
wilaya ya Ruangwa vitaunganishiwa umeme katika Mradi wa Usambazaji Umeme
Vijijini (REA) awamu ya tatu.
Amesema hadi sasa
tayari vijiji 48 vya wilaya hiyo vimeunganishiwa umeme na kwamba lengo lake ni
kuhakikisha vijiji vyote 90 vinapata huduma hiyo, hivyo amewaomba wananchi kuendelea
kuwa na subira.
Waziri Mkuu,
Majaliwa ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na
wananchi wa vijiji vya Michenga, Chinongwe, Makanjiro na Chinokole katika
mikutano ya hadhara aliyoifanya wilayani Ruangwa.
“Niliwaahidi
kuwatumikia, kuwahudumia na kuwasemea ndani na nje ya nchi, nawahakikishia kuwa
sitowaangusha hivyo endeleeni kuwa na subira, nitafanya mambo mengi ya
maendeleo kama isemavyo kauli mbiu yangu, Ruangwa kwa maendeleo inawezekana.”
amesema.
Kwa upande wake
Meneja wa TANESCO mkoa wa Lindi, Sotco Nombo amesema tarehe 15 mwezi huu
wataanza kusambaza vifaa katika kijiji cha Chinongwe na kwamba hadi kufikia
mwezi Mei mwaka huu umeme utakuwa umewaka katika kijiji hicho.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu, Majaliwa amewasisitiza wananchi kuanza kulima kwa
wingi zao la muhogo kwa sababu kuna soko la uhahika la zao hilo baada ya
kujitokeza kwa wafanyabiashara kutoka China na Marekani wanaotaka kununua zao mihogo
nchini.
“Mnataka
hela, mnataka hela? ila lazima mfanye kazi…mimi nimewatafutia hela nawaomba
mlime mihogo kwa wingi maana kuna wafanyabiashara wanataka kununua mihogo, hela
ndiyo hiyo ambayo ni soko la uhakika la mihogo. Nawasihi mchangamkie dili
hili,” amesema.
Amesema
wafanyabiashara hao wanataka kununua mihogo kutoka wilaya za Ruangwa,
Nachingwea na Liwale kwa ajili ya kusaga unga na kutengeneza vyakula vingine
vitokanavyo na zao hilo, hivyo amewaomba wananchi hao kuchangamkia fursa hiyo na
kulima mashamba makubwa ya mihogo.
No comments:
Post a Comment