WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi
kufuatilia maendeleo ya mradi wa umwagiliaji wa Narunyu katika kata ya Kiwalala
wilayani Lindi.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa kata hiyo
kusimamisha msafara wa Waziri Mkuu, Majaliwa katika eneo la Kiwalala jana na
kumuomba awasaidie kuhusu hatma ya mradi wao wa umwagiliaji ambao walitakiwa
wakabidhiwe tangu mwaka 2014.
Awali muwakilishi wa wananchi hao, Mohammed Bakar
alisema kuwa mradi huo uliogarimu shilingi milioni 600 ulitakiwa uwe tayari
umekabidhiwa kwa wananchi, lakini hadi sasa bado na hata banio halijakamilika,
hivyo wanashindwa kuendelea na kilimo katika eneo hilo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu mradi huu bado haujaanza ila
tulishangaa wakati wa mbio za mwenge mwaka 2014 ilisomwa taarifa kwamba wakazi
wa Kiwalala wananufaika na mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Narunyu jambo
ambalo si kweli kwani mradi huu haujawahi kufanya kazi na hata banio hakuna,” amesema.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema malalamiko hayo ya
wananchi wa Kiwalala lazima yafanyiwe kazi, hivyo amemuagiza mkuu wa mkoa wa
Lindi, Zambi kuhakikisha anakwenda kwenye kata hiyo kulipatia ufumbuzi suala
hilo.
“Kweli kuna miradi ambayo inaelekezwa na watu kwa
viongozi kuwa imekamilika wakati bado, namuagiza mkuu wa mkoa kulifanyia kazi
jambo hili,” amesema.
Pia amesisitiza kwamba serikali hii si ya kuleana,
mtu atakayebainika kukwamisha miradi ya maendeleo watamalizana naye hapo hapo,
hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira kwani taarifa yao imepokelewa na
inafanyiwa kazi.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa huo, Zambi amesema tayari
ameshapata taarifa za tatizo la mradi huo na kwamba atafanya ziara kwenye eneo
hilo na mtu atakayebainika kutafuna fedha za mradi huo atamuwajibisha hapo hapo
kwa sababu yeye hataki kutumbuliwa.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
No comments:
Post a Comment