WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amemtaka Mkuu wa Magereza mkoa wa Lindi, kuhakikisha hakuna mtuhumiwa wa dawa za kulevya atakayetoweka katika gereza la mkoa huo.
Amesema kuna watuhumiwa wa dawa za kulevya ambao wanahifadhiwa katika gereza la mkoa wa Lindi hivyo ni vema akajiridhisha kama ulinzi na usalama wa watuhumiwa hao umeimarishwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Majaliwa amemtaka mkuu wa gereza hilo kuwa makini na baadhi ya zabuni wanazozitoa kutoka nje na kuhakikisha ulinzi unaimarisha wakati wote gerezani hapo.
Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo jana (10 Aprili, 2016) wilayani Ruangwa wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Lindi iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa mkoa huo, Godfrey Zambi.
“Mkuu wa Magereza wa mkoa atembee gereza ambalo wanashikiliwa watuhumiwa wa dawa za kulevya na aangalie mradi unaolenga kupeleka maji gerezani hapo kama ni kweli au njia…,” amesema Waziri Mkuu, Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu, Majaliwa amemtaka mkuu huyo wa Magereza kujiridhisha kama ulinzi na usalama wao umeimarishwa na kuhakikisha hakuna mtuhumiwa anayetoweka.
Awali akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu, mkuu wa mkoa wa Lindi, Zambi amesema matumizi ya dawa za kulevya hususan kwa vijana ni miongoni mwa changamoto zinazoukabili mkoa huu ambapo wilaya ya Kilwa inaongoza kwa kuwa na waathirika wengi.
Amesema matumizi ya dawa hizo yanasababisha kupunguza kwa nguvu kazi kwani watumiaji wengi ni vijana, hivyo alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kupiga vita matumizi ya dawa hizo kwa kuwafichua wauzaji na watumiaji.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
No comments:
Post a Comment