HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 08, 2016

WAWAKILISHI WATAKIWA KUISIMAMIA, KUISHAURI SERIKALI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wana jukumu kubwa la kuisimamia na kuishauri Serikali Kuu ili kuhakikisha kwamba matatizo na kero zinazowakabili Wananchi katika maeneo mbali mbali nchini zinatatuliwa kwa ufanisi na mafanikio makubwa.

Alisema Wawakilishi pia wanapaswa kuhakikisha kuwa Serikali inatoa mchango wake kikamilifu katika kuyafanya maisha ya Wananchi wote kuwa bora zaidi kwa kutumia nguvu kazi na rasilmali zilizopo hapa Nchini.

Akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa kwanza wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar huko katika Ukumbi wa Baraza hilo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ina matarajio ya kupata Taarifa na ushauri kutoka kwa Wawakilishi hao juu ya maeneo yatakayohitaji kupewa msukumo ili kuongeza kasi ya
Maendeleo.

Alisema heshima kubwa waliyotoa Wananchi katika kuwachaguwa Wawakilishi hao kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iwe ndio macho na masikio yao katika mategemeo ya kusaidiwa kutatua changamoto zao
mbali mbali za maendeleo zinazowakabili kila siku.

“ Sisi ndio masikio na macho ya Wananchi. Wametupa heshima kubwa kwa kutuchagua kuwa wajumbe wa Baraza hili wakiwa na mategemeo  makubwa kwamba tutawasaidia kutatua changamoto tofauti za maendeleo zinazowakabili ”. Alisema Balozi Seif akiwa ndie mtendaji Mkuu wa
Serikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba waheshimiwa Wawakilishi kwa vile uchaguzi umekwisha warudi Majimboni mwao ili wakashirikiane na Wananchi wao katika kuelekeza nguvu zao kwenye harakati za
maendeleo sambamba na kudumisha amani na utulivu wa Visiwa hivi.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia suala la amani na utulivu kwa nguvu zote ili kutekeleza mipango ya kujiletea maendeleo zaidi ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa.

Balozi Seif alinasihi kuwa hakuna haja ya kukumbushana mambo yaliyopita licha ya kwamba Serikali inatambua wapo baadhi ya Watu wakorofi wanaojihusisha na vitendo vya kuhatarisha amani ya Nchi iliyopo kwa sasa.

Alisema wakorofi hao walijihusisha na utegeji wa miripuko
inayosadikiwa kuwa mabomu na kuchoma moto mashamba ya mikarafuu, nyumba za baadhi ya wananchi pamoja na maskani za Chama cha Mapinduzi.

Alisema vyombo vya dola vinaendelea na hatua ya  uchunguzi wa matukio hayo na baadaye kuchukuwa hatua kwa mujibu wa sheria na kuonya kwamba hakutakuwa na mtu atakayepona kuchukuliwa hatua kali za kisheria iwapo
atabainika kutishia amani na utuliovu wa Taifa.

Akizungumzia  suala la uwajibikaji  katika Taasisi za Umma Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliwaomba Watendajo wote wa Serikali  watakaoteuliwa hapo baadae wakubali kwa moyo wao mkunjufu kuwatumikia Wananchi bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia au Dini.

Balozi Seif alisema Serikali kuu muda wote imekuwa ikihimiza uwajibikaji uliotukuka sambamba na usimamizi mzuri wa fedha na rasilmali nyengine za umma katika ngazi zote.

Alionya kwamba zipo Idara na Taasisi za Serikali zilizooza  sana na kulalamikiwa  na Wananchi kwa sababu ya kutowajibika kwa watendaji wa Taasisi hizo. 

Hivyo amehidi kumsaidia Rais katika kuyatumbua majipu yatakayojitokeza. “ Nawaomba watendaji watakaoteuliwa wasikae maofisini tu, bali wazitemnbelee taasisi zilizo nchini yao ili waone uwajibikaji wa Taasisi hizo. Na mimi naahidi kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuyatumbua majipu yatakayojitokeza ”. Alisema Balozi Seif.

Akigusia tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa  zao katika mfumo wa ubaguzi kwa sababu za itikadi za Kisiasa Balozi Seif  alionya kwamba jambo hilo sio zuri na ingefaa likaachwa mara moja.

Alisema inasikitisha na mambo yanayotokea katika baadhi ya maeneo Kisiwani Pemba ambayo baadhi ya wafanyabiashara hao wameanzisha mtindo wa kuwanyima Wananchi wenzao kuwauzia bidhaa kwa sababu za tofauti za kisiasa.

Balozi Seif alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya  
inalifuatilia kwa karibu suala hilo na kamwe haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mfanyabiashara ye yote atakayebainika kuendeleza jambo hilo ikiwa ni pamoja na kumfutia  mara moja leseni yake ya biashara.

Kuhusu mvua za masika zinnazoendelea kunyesha Balozi Seif  alitoa wito maalum kwa wawakilishi kushirikiana na Wananchi katika kuendelea usafi wa mazingira na kutekeleza maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na  maradhi ya miripuko ukiwemo ugonjwa wa Kipindupindu ambao bado unaendelea kusumbua Jamii.

Alisema mvua hizo ni vyema pia zikatumiwa  vizuri na wananchi hasa wakulima katika kuendeleza shusghuli za kilimocha mazao ya chakula  na biashara kwa lengo la kupata mavuno mengi zaidi na kujiongezea kipato.

Akigusia migogoro ya ardhi iliyoleta changamoto kubwa kwa Serikali katika kipindi kilichopita Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kadhia hiyo kwa kiasi kikubwa imesababishwa na baadhi ya Viongozi kwa sababu ya tamaa.

Balozi Seif alisema hata baadhi ya wananchi wamekuwa wakiendelea na ujenzi holela wa nyumba za kudumu bila ya kibali na wakati mwengine katika maeneo yasiyoruhusiwa kama vile sehemu za vianzio vya maji pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa miji ya kisasa.

Aliwatanabahisha watu wote waliojenga katika maeneo hayo kuacha kufanya hivyo mara moja sambamba na Viongozi wenye tamaa ya fedha au kujilimbikizia maji wajisafishe kabla mkondo wa sheria haujawakumba.

Mapema ndani ya kipindi cha siku mbili  cha Mkutano huo wa Baraza la Wawakilishi  Wajumbe wa Baraza la hilo walipata fursa ya kuijadili Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein aliyoitoa mapema wiki hii wakati akilizindua rasmi
Baraza hilo.

Pamoja na mambo mengine Wajumbe kadhaa wa Baraza hilo walielezea umuhimu wa Wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao Majimboni kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa Taifa  ili kuisimamia ipasavyo Ilani ya Chama kilichopata ridhaa ya kuongoza Dola katika Kipindi cha miaka mitano ijayo ambacho ni CCM.

Wajumbe hao walisema wakati wa kuliandaa Taifa kuelekea katika uchumi wa kati  na kati ifikapo mwaka 2025 nii huu kwa kuchapa kazi kwa bidii na ni vyema wakaepuka tabia mbaya ya kuutumia wakati wao kwa kuendeleza siasa na majungu yanayoweza kuutia doa Mpango huo wa Taifa.

Wakigusia hali ya amani ya Nchi baadhi ya Wawakilishi hao walisema licha ya kwanza udhibiti wa utulivu na amani ni dhamana ya Serikali Kuu, lakini Wananchi katika maeneo yao bado wana wajibu na jukumu la kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi pale wanapoona viashirio vya uvunjifu wa amani.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliopongeza Uongozi wa Baraza la
Wawakilishi uliopita ukiongozwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi
Mstaafu Mh. Pandu Ameir Kificho kwa kuliongoza Braza hilo kwa umakini
mkubwa ndani ya kipindi cha miaka 20 mfululizo.
Alisema Mh. Kificho na viongozi wenzake walitumia hekima, busara na
uvumilivu mkubwa wa kuliongoza Baraza hilo katika muda wote kazi
ambayo wanapaswa kutakiwa kheir na mafanikio katika muda wao wa
baadaye.

Mkutano wa kwanza wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar
umeahirishwa katika Ukumbi wa Baraza hilo Mweni hadi asubuhi ya
Jumatano ya Tarehe 18 Mei 2016 mnamo saa 3.00 za asubuhi.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
08/04/2016.

No comments:

Post a Comment

Pages