HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 13, 2016

TANZANIA YANG’ARA MKUTANO WA KUPAMBANA NA RUSHWA LONDON

*Waziri Mkuu kukutana na Watanzania kesho, atoa ufafanuzi kuhusu Diaspora

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wakuu wa nchini na washiriki wa mkutano wa kimataifa wa kupambana na rushwa wamevutiwa na jitihada ambazo Tanzania imezichukua kukabiliana na janga hilo.

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Mei 13, 2016) wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ushiriki wake kwenye mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Nchi ulioitishwa kujadili suala la kupambana na rushwa duniani uliofanyika Lancaster House, jijini London, Uingereza.

Waziri Mkuu alisema katika kikao cha kwanza kilichohudhuriwa na wakuu wa nchi na viongozi wa kitaifa wapatao 20, alipata fursa ya kuelezea jinsi Tanzania ilivyoweza kupambana na rushwa kwa kuzingatia vigezo vikuu vinne.

Waziri Mkuu alivitaja vigezo hivyo kuwa ni kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria zinazohusu masuala ya rushwa; uanzishwaji wa mahakama maalum ya mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi Julai, mwaka huu; mikakati ya udhibiti wa fedha za miradi ya wananchi na utaratibu wa kubaini wala rushwa kwa kushirikisha jamii ikiwemo kutunza siri za watoa taarifa.

“Ziko sheria ambazo zinafanyiwa kazi hivi sasa ambazo ni lazima zipitishwe na Baraza la Mawaziri kabla mahakama hii haijaanzishwa, zikishapitishwa na Baraza ndipo zitaanza kutumika,” alisema.

Akifafanua kuhusu mikakati ya udhibiti wa fedha za miradi ya maendeleo, Waziri Mkuu alisema kwamba katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imeweza kuongeza kiasi cha fedha zilizotengwa kwa shughuli za maendeleo kutoka asilimia 27 hadi kufikia asilimia 40.

“Kuongezeka kwa kiwango hiki ni ishara tosha  kuwa tumelenga kutoa huduma kwa Watanzania na muhimu katika rushwa ni udhibiti wa fedha hizo na kuhakikisha zinakwenda kwenye miradi; matuizi mazuri ya fedha za Serikali, matumizi mazuri ya fedha zinazochangiwa na wahisani ili ziweze kutekeleza miradi iliyokusudiwa,” alisema.

“Tumekubaliana na uwepo wa uwazi na kushirikishana taarifa hasa katika kupeana taarifa za makampuni yanayoanzishwa na kusajiliwa katika nchi zinazoendelea kama njia ya kudhibiti tabia ya nchi ndogo kama Ireland na Panama kupokea na kuficha fedha zinazotoka kwenye nchi zinazoendelea” alisema.

Alisema kila nchi imesisitizwa kutumia raia na kuwalinda watoa siri, kutumia mifumo ya kiintelijensia, kutumia wanasheria na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya watu wanaokamatwa kwa masuala ya rushwa.

Waziri Mkuu alisema alipata fursa ya kukutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. David Cameron ambaye mbali na kupongeza juhudi za Serikali ya Rais Dk. John Pombe Magufuli katika kupambana na rushwa pia aliahidi kutoa mwaliko ili Tanzania iweze kushiriki kwenye mkutano mwingine wa masuala ya rushwa utakaofanyika Japan, Julai mwaka huu.

“Anataka Tanzania iende kwenye mkutano huo ili ikaelezee mafanikio iliyoyapata katika kukabili suala hili, ili pia nchi nyingine ziweze kuiga utaratibu ambao Serikali imeutumia hadi tukafanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ofisi yake haijahusika na kuandaa mkutano wa wanadiaspora waishio Uingereza kama ambavyo imedaiwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna watu maalum wamechaguliwa kushiriki mkutano huo.

Amesema mkutano huo umepangwa kufanyika kesho (Jumamosi, Mei 14, 2016) na uko wazi kwa Watanzania wote kushiriki ili waje kusikiliza nchi yao imefanya nini na kama kuna masuala yanahitaji ufafanuzi, watapatiwa fursa hiyo.

“Kulikuwa na hofu ya watu wanaotoka mbali kutoweza kushiriki sababu ya gharama, lakini nasema yeyote mwenye uwezo wa kuja aje ndiyo maana tumeuweka muda wa asubuhi ili watu waweze kushiriki na kuwahi kurudi makwao,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, MEI 13, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages