HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 26, 2016

WATU WENYE ULEMAVU WANASTAHILI KUHESHIMIWA-BALOZI SEIF IDD

Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Bibi Abeda Rashid Abdullah aliyenyanyua mkono juu mwenye kilemba chekundu akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais  wa Zanzibar hatua zinazochukuliwa na Idara yake katika kutekeleza majukumu yake. Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu wenye ulemavu Zanzibar Nd. Haidar Ali Madewea wa Pili kutoka Kulia akielezea changamoto zinazolikwaza Baraza hilo wakati uongozi wake ulipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif. Kushoto ya Nd. Madewea ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na kulia yake ni Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye ulemavu Bibi Abeda Rashidd Abdullah. (Picha na OMPR – ZNZ)


              XXXXXXXXXXXXXXX               

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitahadharisha kwamba ubakaji unaowakumba baadhi ya wananchi hasa watu wenye ulemavu nchini  kamwe hautakwisha iwapo jamii itaendeleza tabia za kumaliza wenyewe kwa wenyewe udhalilishaji unaotokea katika familia.

Alisema wananchi wenye ulemavu wanastahiki kuheshimiwa kama watu wengine kwa vile mtihani walioupata walemavu hao ni miongoni mwa majaaliwa ya mitihani ya mwenyezi muungu.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Idara ya Watu wenye ulemavu baada ya kuitembelea Idara hiyo hapo ofisini kwao Migombani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Ziara ya Balozi Seif ilikuwa na lengo la kujitambulisha rasmi baada ya Idara hiyo kuingizwa kwenye Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kutokana mfumo wa mabadiliko ya Wizara na Taasisi za Serikali uliofanyika hivi karibuni.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zitajitahidi kupitia vyombo vyake vya Dola kufuatilia na kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya wahalifu wanaohusika na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameahidi kwamba Ofisi yake itaendelea kushirikiana ipasavyo na Uongozi wa Idara hiyo katika kuona changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu hapa nchini zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Balozi Seif aliwapongeza Viongozi na watendaji wa Taasisi hiyo kwa kazi kubwa wanayoitekeleza katika kuwahudumia wananchi wenye ulemavu katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba licha ya mazingira magumu yanayowakabili kila siku.

Aliuagiza Uongozi wa Taasisi hiyo kuendelea kufanya uratibu wa ukusanyaji wa takwimu za wananchi wenye ulemavu kwa kutembelea mikoa yote ili kupata kujua matatizo yanayowakwaza  na ndio fursa pekee itakayorahisisha njia ya kuwahudumia wananchi hao.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye ulemavu Zanzibar Bibi Abeda Rashid Abdullah alisema licha ya uelewa mdogo kwa baadhi ya familia lakini masuala ya watu wenye ulemavu yamepiga hatua kubwa hapa Zanzibar ikilinganishwa na Tanzania bara na baadhi ya Mataifa Barani Afrika.

Bibi Abeda alisema muamko wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwa sasa umekuwa zaidi hali iliyopelekea kupatikana kwa takwimu ya idadi ya watu wenye ulemavu iliyofikia elfu 16,545 Unguja na Pemba kufuatia usajili uliofanywa kuanzia mwaka 2012.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar alifahamisha kwamba sheria, sera pamoja na kanuni zinazomlinda mtu mwenye ulemavu bado zinaendelea kuwa na utata na kuleta usumbufu kwa kundi hilo la jamii hapa nchini.

Alisema idadi kubwa ya ujenzi wa majengo ya Ofisi za Umma hapa nchini haujazingatia mazingira rafiki yanayotoa fursa kwa watu wenye ulemavu kupata huduma rahisi kwenye baadhi ya ofisi hizo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Watu wenye ulemavu Zanzibar Nd. Haidar Ali Madewea aliziomba Taasisi zinazosimamia utengenezaji wa Sera za Watu wenye Ulemavu kuharakisha rasimu  iliyoandaliwa kwa ajili ya kundi hilo.
Nd. Madewea alisema kazi nyingi zinazosimamiwa na Baraza hilo hasa mfumo wa matumizi ya fedha zinashindwa kutekelezwa kutokana na urasimu uliopo wa utekelezaji wa utaratibu uliopo hivi sasa.

Hata hivyo  Mwenyekiti huyo wa Baraza la Watu wenye Ulemavu alieleza kwamba Baraza hilo litaendelea kuishauri Serikali kuu pamoja na Taasisi zake kuendelea kuwapatia haki na fursa watu wenye ulemavu zikiwemo za elimu na afya.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/5/2016.

No comments:

Post a Comment

Pages