KATIBU MKUU Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu, Bunge na Siasa, Uledi Mussa amesema
atahakikisha michango ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya watumishi wa Ofisi hiyo
inafikishwa kwa wakati.
Kiongozi huyo ametoa kauli
hiyo leo (Jumanne, 21 Juni, 2016) wakati
akijibu maswali ya watumishi wa Ofisi hiyo mjini Dodoma katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma inayoanzia
Juni 16 hadi 23 ya kila mwaka.
Kila mwaka Tanzania
imekuwa ikiungana na mataifa mengine ya Bara la Afrika kuadhimisha Wiki ya
Utumishi wa Umma Barani Afrika ambayo kauli mbiu ya mwaka huu ni Uongozi
wa Umma kwa Ukuaji Jumuishi:kuelekea katika Afrika tunayoitaka.
“Nitafuatilia michango ya
watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha inafika kama
inavyotakiwa na kwa wakati ili hata wanapomaliza muda wao wa utumishi
wasihangaike,” amesema.
Katika hatua nyingine,
Uledi
amewataka Wakuu wa Idara kuandaa mpango
wa mafunzo kwa watumishi na washirikishe kila mtu katika idara husika kabla ya
kuuwasilisha kwake.
Katibu Mkuu aliyasema hayo
wakati akijibu maswali ya baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo, ambapo Anjani
Ngulukia (Msaidizi wa Ofisi) alitaka kupatiwa ufanunuzi kuhusu suala la
michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo imekuwa haipelekwi kwa wakati.
Pia mtumishi mwingine Ernest
Msabalala ambaye ni Mtunza Kumbukumbu Mkuu aliomba ofisi iandae utaratibu wa
kuwa na mafunzo kwa watumishi ili kuongeza ufanisi wa kazi.
No comments:
Post a Comment