HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 19, 2016

ZAIDI YA VIJANA 200 WAPATIWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI

Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana yaliyoandaliwa na taasisi ya kibiashara ya watu wa marekani (AMCHAM-TZ) na kudhaminiwa na Benki M, Deogratius Kilawe akielezea mafanikio aliyoyapata wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)

Na Mwandishi Wetu

 ZAIDI ya vijana  200 wamepatiwa  mafunzo ya ujasiria mali lengo likiwa ni kujua fursa mbalimbali na kuondokana na tatizo la ajira ambalo kwa sasa limekua likiwakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo, muandaaji  Richard Miles,  kutoka taasisi ya kibiashara ya watu wa marekani (AMCHAM-TZ) alisema amefurahi kuona vijana wa kitanzania  walivyojitokeza na kubainisha  matatizo yanayowazunguka ili yaweze kutafutiwa  ufumbuzi.

 Miles alisema mafunzo hayo yatawasaidia vijana hao , kutimiza ndoto zao na kwamba  wengi wao walikuwa hawajui wapi kwa kuanzia ila kwa sasa kutokana na elimu waliyoitoa wataziona  fursa mbalimbali.

Baadhi ya vijana waliopata mafuzo  hayo  ambayo yalifanyika   katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, walisema wamepata njia pekee ya kujihusisha na biashara na kuahidi kuwa,  wako mbioni kumaliza masomo yao ya elimu ya juu.

Janeth Julius mwanafunzi wa elimu ya juu katika chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema amepata mwanga wa jinsi ya kuendelea kuboresha  biashara yake ya kuuza vipodozi.

“Nilikua nikifanya biashara kwa mazoea kwa sababu napenda kujishughulisha na biashara ndogo ndogo  kwa sasa kutokana na mafunzo niliopata, nitaweza kukuza biashara yangu na kuajiri vijana wenzangu ili  tuweze kukuza soko la ajira nchini mwetu na tufikie malengo,”alisema Janeth.

Naye Mkurugenzi wa benki M,Jacqueline Woiso, ambao ni wadhamini wakuu wa mafunzo hayo, alisema amefurahi kuona vijana wengi waliojitokeza kushiriki mafunzo hayo.

Alisema anaamini mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kutimiza ndoto zao kwa namna moja au nyingine, ambapo wanaweza kutumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kutangaza biashara zao.

No comments:

Post a Comment

Pages