HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 20, 2016

RAIS MAGUFULI ATEUA WENYEVITI WANNE WA BODI MBALIMBALI

Na Neema Mwambapa

RAIS John Magufuli amewateua Wenyeviti wanne wa bodi mbalimbali ikiwamo Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) na Bodi ya Shirika la Posta.

Katika uteuzi huo Rais Magufuli amemteua Luteni Kanali Mstaafu Haroun Kondo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania.

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 20 Septemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ilisema kuwa uteuzi wa Luteni Kanali Mstaafu Haroun Ramadhani Kondo ulianza Septemba, 5 mwaka huu.

Kondo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Yamungu Kayandabila ambaye amemaliza muda wake.

Pia  Rais Magufuli alimteua Hedwiga Swai kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuanzia Septemba 5 mwaka huu.
Swai ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimteua Balozi Ladislaus Komba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kuanzia Septemba, 5 2016.

Balozi Komba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Christopher Liundi ambaye amemaliza muda wake.

Halikadhalika, Rais Magufuli alimteua Fidelis Mutakyamilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Matumizi ya ardhi kuanzia  Agosti 5 2016.

Mutakyamilwa ni Mwanasheria Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa LAPF.

No comments:

Post a Comment

Pages