Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa
familia zilipatwa na msiba kufuatia ajali ya basi la Kampuni ya New Force
iliyotokea jana tarehe 19 Septemba, 2016 majira ya saa 2:00 Usiku katika Kijiji
cha Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya Igominyi Mkoani Njombe ambapo watu 12
wamepoteza maisha na wengine 28 kujeruhiwa.
Basi hilo
limepinduka katika kona ya barabara wakati likisafiri kutoka Dar es Salaam
kwenda Songea Mkoani Ruvuma.
Katika salamu hizo
kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi, Rais Magufuli amesema
amepokea taarifa za ajali hiyo kwa masikitiko makubwa na kwamba anaungana na
familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopatwa na msiba katika kipindi
kigumu cha majonzi.
"Ndugu Mkuu
wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi naomba unifikishie pole nyingi kwa wote
walipatwa na msiba, wamewapoteza wapendwa wao, wamewapoteza watu waliowategemea
na hakika familia zimetikisika.
"Sote
tuwaombee wote waliofikwa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na
ustahimilivu na pia tuwaombee Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi,
Amina" Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia
amewapa pole majeruhi wote na amewaombea wapone haraka ili waweze kuungana na
familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
20
Septemba, 2016
No comments:
Post a Comment