Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarest Ndikilo baada ya kuwasili kwenye eneo inapojenjwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha kuzindua Mpango Mkakati na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ya Tanzania Septemba 21, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Ametoa wito huo leo (Jumatano, Septemba 21, 2016) wakati akizindua Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2015-2020) na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ya Tanzania kwenye eneo inapojengwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Waziri Mkuu amesema wananchi wengi wanapata shida ya kufikia huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za mahakama katika ngazi ya kata na wilaya jambo ambalo halikubaliki.
“Nichukue fursa hii kuwakumbusha wenzetu wa mahakama kuwa, sisi sote tupo kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania, hivyo mipango na mikakati yetu iangalie utaratibu utakaotoa haki kwao ili kuwaongezea imani kwa Mahakama na Serikali kwa ujumla,” amesema.
Amesema mpango mkakati aliouzindua leo ni dalili nzuri ya uongozi na utendaji wa Mahakama ambayo inajitambua, inajua inataka kwenda wapi na kwa muda upi na kuweka utaratibu wa kujipima na kujitathmini kwa kila hatua.
“Naamini mtajielekeza vizuri katika utekelezaji wa Mpango Mkakati huu na kimsingi Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli ipo bega kwa bega nanyi na inaunga mkono jitihada zote za kuimarisha Mahakama.”
Waziri Mkuu pia alizindua Mpango Mkakati wa mwaka 2015/16 – 2019/20 na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ya Tanzania unaohusisha wilaya ya Kibaha, Mkuranga na Bagamoyo. Mradi huo utakaogharimu sh. bilioni 139.5 (sawa na dola za Marekani milioni 65) utagharimiwa kwa fedha kutoka katika bajeti ya Serikali na mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Amesema Serikali itahakikisha fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia katika mradi huo zinatumika kwa uaminifu mkubwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa fedha ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira iliyohudhuria uzinduzi huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande alisema mahakama imeanzisha kada mpya ya watumishi wa kusimamia masuala ya fedha ili kada ya sheria iendelee na shughuli za mahakama tu.
Alisema kuzinduliwa kwa mpango mkakati wa mwaka 2015/16 hadi 2019/20 pamoja na na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ya Tanzania kutaiwezesha mahakama kujenga mahakama Kuu kati ya tano hadi saba katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Alisema kati ya mikoa 26 nchini, ni mikoa 14 tu ambayo ina Mahakama Kuu na kwamba mahakama hizo zinaweza kujengwa kwenye mikoa ya Njombe, Geita, Simiyu, Katavi, Singida, Manyara, Songwe, Lindi, Pwani na Morogoro.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema amefarijika na hatua na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Hussein Katanga kwa kuamuakushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) katika kuhakikisha kuwa Mtanzania wa kawaida anasogezewa huduma za kisasa za mahakama kwenye majengo yenye ubora wa hali ya juu yatakayowezesha utoaji wa huduma kwa haraka na gharama nafuu.
Amesema uamuzi wa kukitumia Chuo cha Ardhi ni wa busara sana kwani umepunguza gharama za ujenzi kwa zaidi ya sh. milioni 800 kwa kutumia teknolojia ya ujenzi wa nyumba na Ofisi kwa gharama nafuu ijulikanayo kama Moladi.
“Mheshimiwa Katanga aliamua kutagaza zabuni na katika waliojitokeza, wa kwanza alitaka kujenga kwa sh. bilioni 1.73, wa pili alitaka sh. bilioni 1.55 na wa tatu alitaka sh. bilioni 1.3.”
“Lakini Chuo cha Ardhi kwa kimetumia gharama ya sh. milioni 550 tu, sasa kwa nini tusijifie watu wa aina hii? Na ndiyo maana Profesa Mshoro (Makamu Mkuu wa Chuo) ni miongoni mwa watu walioko kwenye Kamati ya kuishauri Serikali juu ya ujenzi mpya wa Mji Mkuu wa Dodoma,” alisema.
Amemtaka Prof. Mshoro aimarishe kitengo chake cha ujenzi ili kiweze kuendana na kasi ya mahitaji hasa katika suala la ujenzi wa makzi na Ofisi Dodoma. Pia amemshauri awasiliane na Benki ya Rasilmali (TIB Corporate na TIB Development) ili kupata ushauri wa mitaji ya kufanya kazi kubwa kubwa.
“Imarisha kitengo chako cha ujenzi ili upate Vijana wengi wa kusimamia miradi hasa ya ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi, hospitali na vituo vya afya ambavyo mahitaji yake ni makubwa hapa nchini,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
JUMATANO, SEPTEMBA 21, 2016
No comments:
Post a Comment