Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amempongeza Balozi Prof. Joram
Mukama Biswaro kwa kuteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Kamisheni
ya Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja huo Sudan Kusini.
Balozi Prof. Joram
Mukama Biswaro ameteuliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU)
Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Brigedia
Jenerali Sara Thomas Rwambali ambaye amemaliza muda wake.
Katika pongezi
hizo Rais Magufuli amesema Tanzania imepokea uteuzi huo kwa heshima kubwa na
ipo tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitaji kwa Balozi Joram Mukama
Biswaro katika utekelezaji wa majukumu yake.
"Natambua
kazi kubwa iliyopo mbele yako katika nafasi hiyo muhimu ndani ya Umoja wa
Afrika (AU), hata hivyo kwa kutambua uwezo wako, uzoefu wako na uchapakazi wako
naamini kuwa utatekeleza majukumu yako kwa viwango vya hali ya juu na
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma
hatajutia uamuzi wake wa kukuteua katika nafasi hiyo"
amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli
amemtakia heri Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro katika majukumu hayo mapya, na
amemshukuru na kumpongeza Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali aliyemaliza
muda wake kwa uwakilishi mzuri katika kipindi chake.
Aidha, Rais
Magufuli ambaye ndiye aliyempendekeza Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro kushika
nafasi hiyo, amemshukuru Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Dkt.
Nkosazana Dlamini-Zuma kwa kuridhia mapendekezo yake.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
04 Oktoba,
2016
No comments:
Post a Comment