HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 08, 2016

CTI yazindua shindano Tuzo za kampuni Dar

NA MWANDISHI WETU

SHIRIKISHO la Viwanda Tanzania (CTI), kwa kushirikiana na Bank M, jana walizindua shindano la Tuzo za Rais za mzalishaji bora viwandani (PMAYA) 2016 linalofanyika jijini Dar es Salaam na kuwaalika kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa tuzo hizo.


Akitangaza shindano hilo katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi wa mwaka, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanya Tanzania (CTI), Leodegar Chilla Tenga alisema wanafanya hivyo katika kutekeleza ushauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli na mlezi wa CTI.


Tenga, aliyewahi pia kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema safari hii wao CTI wameamua kupanua wigo wa ushiriki kwa kualika hata kampuni ambazo si wanachama.


“Ni tumaini letu kuwa kuzishirikisha kampuni zisizo wanachama katika shindano la mwaka huu kutasaidia  kuongeza idadi ya washirik, hivyo kulifanya shindano kuwa la kiushindani zaidi,” alisema Tenga.


Shindano hilo lililoanza mwaka 2005, limekuwa likifanyika kila mwaka kuzawadia wenye viwanda  waliofanya vizuri kwa mwaka uliopita. Zawadi hizi zilianza  kutolewa  kwa washindi kwa mara ya kwanza  mwaka 2005, pale CTI ilipoandaa  hilo nchi nzima.


Kuhusu shindano la mwaka huu, Tenga alisema limeboreshwa zaidi  kwa kuingiza katika shindano hilo zawadi ya matumizi bora ya Nishati.


Alisema, zawadi hiyo inalenga kuhamasisha washiri kuhusu  umuhimu wa kufanyakazi kwa kuzingatia matumizi bora ya nishati ya viwandani.


Tenga alisema, CTI, DANIDA na GIZ kwa upande wao wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha  usimamizi  na matumizi bora ya nishati viwandani kwa mfano ukaguzi wa nishati.


Tenga aliongeza kuwa, lengo la shindano hilo ni pamoja na kutambua nafasi na mchango wa sekta  ya viwanda  katika  uchumi wa taifa, kuhamasisha na kuvutia wawekezaji katika sekta  ya viwanda.


Alisema, lengo jingine ni kutangaza umuhimu  wa sekta  ya viwanda nchini na kuinua viwango vya kufanya  biashara na kuchochea utawala  bora  katika makampuni nchini.
Pia, ni kutambua na kuthamini  nafasi na umuhimu wa sekta ya  viwanda katika maendeleo ya kitaifa.


Kuzinduliwa kwa shindano la mwaka huu la PMAYA 2016, kumetoa fursa kwa wanachama na wasio wanachama wa CTI kutumiwa dodoso kwa barua pepe, kuzijaza na kutuma kwa CTI kwa ajili ya kufanyiwa tathmini.

No comments:

Post a Comment

Pages