Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kushoto) akitoa maagizo kwa wakandarasi
kutoka Kampuni ya KALPATARU, inayojenga Mfumo wa Usafirishaji Umeme katika
Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea, kufanya kazi usiku na mchana ili
ikamilishe kazi hiyo kwa muda uliopangwa ambao ni miezi minne kutoka sasa. Wa
pili kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mkuu wa
Wilaya ya Songea Palolet Mgema.
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa
Kanuti Punguti ambaye ni Meneja wa Kituo cha kufua umeme kilichopo Lizaboni,
Songea alipotembelea Kituo hicho jana, akiwa katika ziara ya kazi kukagua
utekelezaji wa Miradi ya Umeme katika Mkoa wa Ruvuma. (Picha na Veronica Simba,
Songea).
Na
Veronica Simba - Songea
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani ameiagiza Kampuni ya Ukandarasi ya
KALPATARU inayojenga Mfumo wa Usafirishaji Umeme katika Mradi wa Umeme wa
Makambako – Songea, kufanya kazi usiku na mchana ili ikamilishe kazi hiyo kwa
muda uliopangwa ambao ni miezi minne kutoka sasa.
Dkt Medard Kalemani
aliyasema hayo jana mkoani Ruvuma akiwa katika ziara kukagua utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya umeme na madini.
Akikagua maendeleo ya
kazi husika katika maeneo ambayo panajengwa miundombinu ya usafirishaji umeme
na vituo vya kusambazia umeme vya Mradi huo mjini Songea, Naibu Waziri
aliwataka Maofisa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanaosimamia Mradi huo
kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi husika ili kuhakikisha wanakamilisha kazi
hiyo kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.
“Ninawataka mfanye
kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi yenu kwa wakati kwani hatutatoa muda
wa nyongeza,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi,
Naibu Waziri alibainisha kuwa, muda uliopangwa kukamilisha kazi ya ujenzi wa
mfumo wa usafirishaji umeme ni Machi 2017.
Aliongeza kuwa ni
lazima kazi hiyo ikamilike kwa wakati ili kutoa fursa kwa kazi ya ujenzi wa
miundombinu mingine ya usafirishaji umeme kukamilishwa kufikia mwezi Desemba
mwakani na hivyo kuwezesha shughuli zote kukamilika ifikapo Juni 2018 na
wananchi kupata umeme ifikapo mwezi Septemba mwaka huo kama ilivyopangwa.
Kwa upande wa
miundombinu ya usambazaji umeme, Dkt Kalemani alisema kuwa, Mkandarasi husika
ambaye ni Kampuni ya ISOLUX anatakiwa kuwa amekamilisha ujenzi wake ifikapo
mwezi Mei, 2017.
Alisema kuwa, kazi
hiyo ni kubwa na itahusisha takribani kilomita 300 ambapo wateja wanaotarajiwa
kuunganishwa ni 13,000 na hivyo kutatua matatizo ya umeme kwa Mkoa wa Ruvuma.
Kuhusu utekelezaji wa
Mradi wa Umeme Vijijini wa REA II mkoani Ruvuma, Dkt Kalemani alisema kuwa,
mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 kwa kazi ya kuweka miundombinu lakini
wapo wateja ambao hawajaunganishiwa umeme.
Aliwataka wataalam
husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Tanesco, kuhakikisha wateja
wote ambao wameshalipia umeme waunganishiwe nishati hiyo ndani ya mwezi huu wa
Desemba ili kuruhusu REA III kuanza pasipo mabaki ya kazi za REA II.
Mradi wa Makambako –
Songea unatekelezwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results
Now-BRN) na unalenga kuunganisha umeme kutoka Makambako hadi Songea na
kunufaisha wananchi katika maeneo husika yaani mikoa ya Njombe na Ruvuma.
Mradi huo ni wa umeme
wa kilovolti 220 kwa umbali wa kilomita 250 na umelenga kuwanufaisha watu
22,700 katika vijiji 120 vya maeneo husika.
No comments:
Post a Comment