HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 01, 2016

SH. BILIONI 40 ZIMEPELEKWA WIZARA YA AFYA KWA AJILI YA UNUNUZI WA DAWA NA VIFAA TIBA - MAJALIWA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (katikati) na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Richard Kwitega baada ya kuwasili jijini Arusha kuanza ziara ya kazi mkoani humo Desemba1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo.
 Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Monduli, Iddi Kimanta.
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia sasa, Serikali imekwishaipatia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto sh. bilioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba iliyokuwa inazikabili hospitali mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Desemba Mosi, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Manyara aliposimama wilayani Babati akiwa njiani kwenda Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku saba inayotarajiwa kuanza kesho.

Amesema suala la dawa kwa sasa linaenda vizuri, hivyo amewataka viongozi wa mikoa kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinavyopelekwa katika hospitali zao zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Suala la dawa linaenda vizuri sasa. Hakikisheni mnadhibiti mianya ya upotevu wa dawa kwenye hospitali zetu kwa kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wa sekta ya afya wasiokuwa waaminifu,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kuweka utaratibu wa kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa pamoja na kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuwawezesha kupata huduma ya matibabu bure kwa mwaka mzima.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuachana na mila potofu na badala yake wawasomeshe watoto wao hasa wa kike kwani suala la elimu mkoani Manyara bado halijapewa kipaumbele.

Hakikisheni watoto wote waliofaulu kwenda kidato cha kwanza wanakwenda shule ifikapo Januari. Maofisa Elimu shirikianeni na halmashauri kuhakikisha jambo hili linafanikiwa kwaasilimia 100,” amesema.

Akizungumzia kuhusu suala la utoro na mimba kwa watoto wa kike, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kudhibiti jambo hilo kwa kuwachukulia hatua za kisheria wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, DESEMBA MOSI, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages