Benki ya CRDB imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya zawadi kwa wateja wake watakaofanya miamala na malipo kupitia huduma ya SimBanking, ikiwa ni sehemu ya kampeni maalum ya kuwahamasisha matumizi ya huduma hiyo ya kidijitali.
Katika kampeni hiyo, mshindi wa kwanza katika droo ya mwisho atajipatia shilingi milioni 30, huku mshindi wa pili akipata milioni 20 na wa tatu milioni 10. Mbali na fedha taslimu, washindi wengine watajishindia zawadi mbalimbali ikiwemo safari za kwenda nje ya nchi, kutembelea mbuga za wanyama, vocha za manunuzi pamoja na vifaa kama simu za mkononi na kompyuta mpakato.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya SimBanking Kimpango Wako, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, alisema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwapa motisha wateja pamoja na watoa huduma kutumia zaidi mifumo ya kidijitali katika miamala yao ya kifedha.
Alieleza kuwa zawadi hizo zitatolewa kupitia droo zitakazokuwa zikifanyika kila wiki, kila mwezi pamoja na droo za kila robo mwaka, ili kuongeza nafasi kwa washiriki wengi kushinda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wateja wa Awali na Wakati wa benki hiyo, Bonaventure Paul, alibainisha kuwa aina mbalimbali za miamala ikiwemo malipo ya huduma, uhamishaji fedha na matumizi ya kila siku kupitia SimBanking zitamuwezesha mteja kushiriki na kupata nafasi ya kushinda katika kampeni hiyo.






No comments:
Post a Comment