TANZANIA imeandika ukurasa mpya katika historia ya elimu ya ufundi kwa kupeleka walimu 150 wa Amali za Kihandisi nchini India.
Hatua hii kubwa ya kimkakati siyo tu safari ya mafunzo, bali ni uwekezaji wa kitaifa katika mustakabali wa elimu na uchumi wa viwanda, ikilenga kuongeza umahiri wa walimu na kuandaa kizazi cha wataalamu watakaoshindana kimataifa katika nyanja za teknolojia na uhandisi.
Katika hafla ya kuwaaga walimu hao Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesisitiza kuwa mpango wa mafunzo hayo ni utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima ya miaka 10, unaolenga kujenga umahiri wa ufundishaji na kuandaa kizazi cha wataalamu wenye ushindani wa kimataifa. Ameeleza kuwa safari ya mageuzi ya elimu inaendelea na haitarudi nyuma, huku akiwataka walimu watambue nafasi yao kama daraja kati ya sera na utekelezaji darasani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amewataka walimu hao kudumisha nidhamu na maadili, kujifunza kwa bidii na wakirudi wasambaze maarifa kwa wenzao ili kuharakisha mageuzi ya elimu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia walimu hao fursa ya mafunzo, akisisitiza kuwa ni ishara ya dhamira ya dhati ya kuendeleza mageuzi ya elimu, huku akipongeza mshirikiano wa viongozi wa wizara za kisekta katika kulitekeleza kwa ufanisi.
Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa ameeleza kuwa mafunzo hayo ya mwezi mmoja yamewahusisha walimu kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na viongozi wa ngazi ya elimu mkoa kutoka mikoa tisa ili kusimamia kikamilifu uendelevu wa mafunzo warudipo nchini.
Wanufaika wa mafunzo hayo, akiwemo Mwalimu Judith Faustine wa Uhandisi Ujenzi katika Shule ya Sekondari Mwadui Ufundi na Mwalimu Jacob Mwalyego wa fani ya Uashi katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mbogwe, wameishukuru Serikali kwa kuwapatia nafasi hii ya kipekee. Wamesema ni heshima kubwa na fursa ya kuongeza maarifa yatakayowawezesha kuendeleza mageuzi ya elimu nchini.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment