NA MWANDISHI WETU
IMEELEZWA kuwa Nchi za Afrika zimekuwa zikifanya udanganyifu katika utoaji ripoti wa maendeleo yake kiuchumi ili ziweze kushika nafasi nzuri huku wananchi wake wakiishi katika hali duni ya maisha.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) Alvaro Rodliguez ambaye pia ni mtaalamu wa maswala ya uchumi katika uzinduzi wa ripoti ya ukuaji uchumi kwa Nchi 48 zinazoendelea ikiwamo Tanzania na Angola.
Aliitaja Nchi ya Nigeria kama miongoni mwa nchi zilizofanya hivyo ambapo alisema hatua iliwasaidia kushika nafasi ya kwanza katika nchi zenye uchumi mzuri Afrika ilihali wananchi wake wakiishi katika hali duni ya maisha tofauti na Afrika Kusini ambayo inashika nafasi ya pili.
“Nchi za Afrika zimekuwa zikidanganya kuhusu mapato yake na kuzifanya zionekane zina hali nzuri ya uchumi wakati hali halisi ya maisha ya wananchi wake ikiwa mbaya moja ya Nchi hizo ni Nigeria” alisema Rodliguez.
Alisema katika utafiti huo wa uchumi walizingatia mambo makuu matatu ikiwa ni pamoja na wingi wa idadi ya watu katika nchi husika, Ubora wa elimu inayotolewa na fursa za ukuzaji uchumi.
Aliongeza kuwa ili nchi iweze kuonekana ina maendeleo lazima wananchi mmoja mmoja waonekane wana hali nzuri kimaisha kwani haiingii akilini Nchi kusifia uchumi wake umekuwa alafu wananchi wake wakiishi maisha duni.
“Mpango wa maendeleo unahimiza wote kwenda sawa asiwepo aliyeachwa nyuma lakini kwa Nchi zetu hii imekuwa tofauti, wanachama wamekuwa wakieleza uchumi wao kukua lakini hakuna vielelezi vinaoonekana kudhihirisha hilo” alisema.
Naye Matjobhi Riba kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa katika Biashara na maendeleo (UNCTAD), alisema ili taifa liweze kufikia malengo ya millennia ya miaka mitano ni lazima zikaimarisha ukusanyaji mapato, kutengeneza fursa pana za wananchi kujipatia fedha pamoja na kuwa na usimamizi mzuri kwa kiasi cha fedha kinachokusanywa.
No comments:
Post a Comment