Diwani wa Kata ya Buguruni,Adamu Fugame (Cuf) akishirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala,Msongela Palela na Katibu Tawala wa wilaya hiyo,Edward Mpogolo (kulia) wakifanya usafi katika maeneo ya buguruni kwa malapa kutimiza kauli ya Rais Dk.John Magufuli ya kufanya usafi kila mwisho wa wiki ya mwezi jijini Dar es Salaam. (PICHA NA ELISA SHUNDA)
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala,Msongela Palela akizungumza na wananchi wa eneo la Buguruni kwa Malapa na Darajani kuhusu kufanya usafi katika maeneo yanayowazunguka ili kujikinga na kujiepusha na magonjwa ya milipuko kama Kipindupindu baada ya kufanya usafi kutekeleza agizo la Rais Dk.John Magufuli ya kufanya usafi kila mwisho wa wiki ya mwezi jijini Dar es Salaam juzi. Kulia ni Diwani wa Kata ya Buguruni,Adamu Fugame (Cuf) na Katibu tawala wa wilaya hiyo,Edward Mpogolo.
NA EMERISIANA ATHANAS
DIWANI wa Kata ya Buguruni wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Adam Fugame ameagiza viongozi wa kata akiwemo Ofisa Afya, kuwakamata na kuwachukulia hatua watu wasiofanya usafi au kuchangia kwaajili yakuzolewa uchafu.
Akizungumza jijini hapa jana, wakati wa zoezi la ufanyaji usafi ulioshirikisha viongozi mbalimbali wa Manispaa ya Ilala akiwemo Mkurugenzi Msongela Palela, alisema ni vema viongozi wakafanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuwashughulikia watu hao.
"Suala hili sio rai bali tufanye kama sheria ili kufanikisha zoezi la kuimarisha usafi katika maeneo yetu, kwani tusipofanya hivi hakuna litakalotekelezwa, watu hawafanyi usafi," alisema.
Kutokana na umuhimu wa kufanya usafi alisema ni vema watakaokutwa hawachangii wala kujishughulisha na kufanya usafi wakachukuliwa hatua na kutozwa fedha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Palale alisema kuwa katika kata tisa zilizoko katika manispaa hiyo kata ya Buguruni ndiyo imekuwa na ugonjwa wa kipindu pindu ambacho husababishwa na hali ya uchafu.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wakazi wa kata ya Buguruni kuhakikisha wanafanya usafi na kuwa walinzi katika kuhakikisha wanalinda mazingira na kuimarisha usafi kwenye maeneo yao.
No comments:
Post a Comment