Dar es Salaam, Ijumaa, Februari 24, 2017:
Kumekuwa na habari
zinazoenea na kujirudia sana katika mitandao ya kijamii kuhusu hali ya afya ya
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Alli Hassan Mwinyi. Taarifa hizo ambazo
hazieleweki lengo lake, zimekuwa zikidai kuwa Mzee Mwinyi amefariki dunia.
Tutautaarifu umma kuwa
habari hizo si za kweli, ni za kupuuzwa. Mzee Mwinyi ni mzima wa afya, anaendelea
na majukumu yake kama kawaida ambapo jana Alhamisi amehudhuria chakula cha
jioni kuadhimisha siku ya Taifa la Kuwait na leo mchana alitarajiwa kwenda kumjulia
hali Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya.
Natumia fursa hii
kuendelea kuwakumbusha watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa waliobuni
teknolojia hii walikuwa na malengo adhimu ya kumpatia mwanadamu uwanja na
uwanda mpana wa mawasiliano-tusiwachezee shere wabunifu hao kwa kuitumia
kinyume cha malengo.
Aidha, jamii ifahamu
kuwa ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mitandaoni,
2015, kwa mtu yeyote kutangaza, kuchapisha au kueneza habari za uongo au uzushi
katika mitandao.
Kwa niaba ya Serikali nachukua fursa hii kuwapa pole
familia ya Mzee Mwinyi na watanzania wengine kwa mshtuko walioupata kutokana na
uzushi huu. Katika hili hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya
watakaobainika kuhusika na uhalifu huu.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali
No comments:
Post a Comment