Dodoma, Jumamosi, 4 Februari, 2017:
Serikali imesisitiza kuwa,
utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha robo ya kwanza yanaakisi dhamira ya
kimageuzi iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano. Wakijibu hoja
zilizotokana na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na maoni ya
Wabunge Bungeni leo, Mawaziri wa sekta mbalimbali wamesisitiza kuwa kuna
mabadiliko makubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Dhamira ya Rais Iko Wazi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Mhe. January Makamba, amesema kuwa ikiwa ni miezi 15 tu
madarakani, kuna mabadiliko makubwa katika kila eneo la utendaji wa Serikali ya
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Alisema hali hiyo inatokana na dhamira safi
na ya wazi ya Mhe. Rais Magufuli kuenzi misingi aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
Waziri Makamba amesema
miezi 15 baadaye, na Bunge likiwa linajadili takwimu za robo ya kwanza tu ya
Bajeti ya sasa, hata kama wapo watu ambao huenda wameumizwa na mageuzi
yanayoendelea, kwa vyovyote vile, hakuna hoja wala ushahidi wa kulalamika kuwa
nchi inarudi nyuma.
Biashara Zashamiri
Wizara ya Fedha imetoa
takwimu kuonesha kuwa biashara nchini zinashamiri tofauti na baadhi ya watu
wanaotumia takwimu za kufungwa kwa baadhi ya biashara hizo. Wakichangia hoja,
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Phillip Mpango na Naibu wake, Mhe. Dkt
Ashatu Kijaji, wamefafanua kuwa mapato ya Serikali yameongezeka na hali ya biashara
inakwenda vyema.
Akifafanua kuhusu kushamiri
kwa biashara nchini, Naibu Waziri Dkt. Ashatu amesema wakati takwimu
zinaoonesha kuwepo kwa biashara 4,183 tu zilizofungwa, watanzania wengi zaidi wamefungua biashara.
Amesema kuwa takribani biashara 139,554 zimefunguliwa katika mwaka mmoja
uliopita.
Idadi ya Watalii Yaongezeka
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Prof. Jumanne Maghembe amesema kuwa, ubunifu wa kodi mpya zilizoanzishwa
na Serikali haujapunguza idadi ya watalii nchini. Alisema sekta hiyo inayochangia
asimilia 17.5 ya pato la Taifa kwa mwaka baada ya kuanza kukata kodi mpya ya
ongezeko la thamani katika sekta hiyo.
“Mheshimiwa Spika pamoja na
Tanzania kuanza kutoza kodi hii mpaka sasa ninayofuraha kuwajulisha kuwa
hatujaona ushahidi wa kodi hii kupunguza idadi ya watalii wanaokuja nchini,”
alisema Prof. Maghembe.
Mfumo Mpya wa Mbolea
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Tate Ole-Nasha, amesema Serikali
itaanzisha mfumo mpya utakaosaidia kuboresha upatikanaji na usambazaji wa
mbolea nchini.
Amedokeza kuwa, katika
mfumo mpya, Serikali itaanza kununua mbolea kwa ununuzi wa pamoja kama ilivyo
katika ununuzi wa mafuta. Ameongeza kuwa pia Serikali imebaini changamoto ya kuwepo
kwa tozo nyingi katika sekta ya kilimo na kuahidi kuwa itawasilisha Bungeni
hoja ya kupunguza baadhi ya kodi hizo.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment