MBUNGE wa Simanjiro, Mheshimiwa James Ole Millya ametoa pongezi kwa viongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa jinsi wanavyojali na kuwahudumia wananchi.
Ametoa pongezi hizo jana (Alhamisi, Februari 16, 2017) kwenye mikutano miwili ya hadhara iliyofanyika Orkesumet na Mererani wilayani Simanjiro, Manyara, baada ya kupewa nafasi asalimie wananchi kabla Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hajazungumza na wakazi wa maeneo hayo.
“Serikali hii ina viongozi wachapakazi akiwemo Waziri Mkuu. Kwa mara ya kwanza katika jimbo hili, wananchi watapata maji safi kupitia mradi wa maji kutoka mto Ruvu unaoendelea kujengwa hivi sasa,” alisema kwenye mkutano wa hadhara wa Orkesumet.
Alitumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mkuu afuatilie suala la ujenzi wa hospitali ya wilaya kwani sasa hivi wanategemeakituo cha afya na hali ikibadlika inabidi mgonjwa apeekewe Arusha mjini ambako ni umbali wa km. 150 kutoka Orkesumet yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.
Pia aliomba ijengwe barabara ya lami ya kuunganisha wilaya hiyo pamoja wilaya jirani za Hai na Kiteto.
Akiwa Mererani, Bw. Ole Millya aliipongeza Serikali kwa kujenga barabra ya lami kutoka uwanaja wa ndege wa KIA hadi Mererani. Hata hivyo, aliiomba serikali iongeze juhudi ili barabara hiyo iweze Mererani na Orkesumet.
Akihibu hoja hizo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza mbunge huyo kwa uungwana wake wa kutambua juhudi ambazo Serikali imezifanya kwa wananchi wa jimbo lake.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara, aliwaambia wakazi hao kwamba Serikali itaendelea kufanya nao kazi bila kumbagua mtu yeyote kwa sababu ya itikadi za kisiasa.
“Mmempa yeye dhamana ya kuwawakilisha kama mbunge wenu lakini dhamana ya kuongoza nchi mmempa Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kuwapigia kura. Kwa hiyo, kazi yetu ni kuwatumikia ili tutatue kero zinazowakabili wana-Simanjiro,” alisema.
Akizungumzia sekta ya afya, Waziri Mkuu alisema kituo cha afya cha Orkesumet kimepokea sh. milioni 49 kati ya sh. milioni 57 zilizoombwa ili kukiimarisha katika utoaji wa huduma za tiba.
“Tumeshatuma fedha nyingine sh. milioni 163 kati ya sh. milioni 190 zilizoombwa ili kununulia dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Pia kun ash, milioni 483 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya vijijini,” alisema.
“Nia yetu ni kujenga hospitali kubwa ya wilaya lakini ni lazima tuimarishe miundombinu ya utoaji tiba ili wananchi wapate huduma stahiki. Ombi la hospitali ya wilaya nimelipokea na nitafuatilia kujua limefikia hatua gani,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa barabara za kuunganisha wilaya, Waziri Mkuu alisema Serikali itaanza kufanya upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha – Kiteto – Kongwa ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Kuhusu migogoro ya ardhi iliyotajwa na wananchi kwenye mabango yao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Eng. Zephania Chaula aende na mbunge huyo kwenye maeneo yanayolalamikiwa na wananchi ili akabaini chanzo cha migogoro na aitafutie ufumbuzi.
Kuhusu umeme, Waziri Mkuu alisema vijiji 18 katika ya 57 vya wilaya vimeshapatiwa umeme na vilivyoakia vimeshaingizwa kwenye mpango wa serikali wa kuvipatia umeme vijiji 8,000.
Aliwaonya wakazi wa Mererani wachukue tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwani takwimu zinaonyesha kuwa kasi ya maambukizi katika mji huo iko asilimia 18 kiwango alichosema ni kikubwa kuliko kiwango cha kitaifa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, FEBRUARI 17, 2017.
No comments:
Post a Comment