Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kukubali kuendelea kufadhili miradi ya maendeleo ya kipaumbele hususani ya ujenzi wa barabara na usafirishaji wa umeme ili kufungua fursa za kiuchumi katika kanda ya Magharibi.
Dkt. Mpango ametoa shukrani hizo alipokutana na Wakurugenzi Watendaji 12 wanaowakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuharakisha kazi za upembuzi yakinifu na hatimaye kutoa fedha ili utekelezaji wa miradi ya Maendeleo kuanza mapema iwezekanavyo.
Amesema kuwa Benki hiyo iliahidi kutoa fedha ili kujenga barabara ya Nyakanazi, kupitia Kibondo, Kasulu hadi Manyovu, kwa kiwango cha lami na kwamba mradi huo ukipatiwa fedha na kukamilika kwa wakati kutasaidia kuchochea biashara ya wakazi wa maeneo hayo na Nchi jirani ya Burundi.
Pia mradi wa North – West grid wa kusafirisha Nishati ya Umeme kutoka Shinyanga hadi Mbeya kupitia Kigoma Katavi na Rukwa. Mradi huu utawezesha Mikoa ya ukanda wa Magharibi kupata Nishati ya uhakika ya umeme na kufungua fursa za Maendeleo mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati.
“Katika kikao hicho tumewaeleza Wakurugenzi hao wa AfDB hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua katika kutatua changamoto ya Miundombinu ya Umeme na Barabara, kupanua fursa za Ajira, na kuharakisha maendeleo ya ukuaji wa Sekta ya Kilimo ambayo inategemewa na wananchi wengi” Alifafanua Waziri Mpango.
Aidha amewaeleza wageni juu ya jitihada za Serikali ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli za kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, kupambana na rushwa na biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Waziri Mpango ametumia fursa hiyo kuomba AfDB kusaidia kujenga uwezo wa Tanzania kukabiliana na majanga yakiwemo ya matetemeko ya ardhi, ajali kubwa za majini na kwenye migodi. Maeneo mengine ambayo AfDB imeombwa kuisaidia Tanzania ni uvunaji wa rasilimali za bahari (blue economy), kuelekeza mitaji katika Sekta ya kilimo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia nchi.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameipongeza Benki ya AfDB kwa kuwa mdau mkubwa wa Maendeleo ya nchi za Afrika na hasa Tanzania kwa kuwa imekuwa mnufaika mkubwa wa program/ miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wageni hao watakapokuwa wakitembelea miradi mbalimbali inayogharamiwa na AfDBi katika siku takribani tano ambazo watakuwepo nchini
Kwa upande wa Wakurugenzi Watendaji wa AfDB wanaoziwakilisha nchi zao, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mafanikio ya kiuchumi kwa kuwa Tanzania imekuwa na viashiria vingi ambavyo vinaonesha uchumi wa Taifa ni imara ukilinganisha na nchi nyingine katika bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.
Aidha wameitaka Tanzania kuendeleza jitihada za kupambana na Umaskini hasa katika maeneo ya vijijini na kuongeza fursa za ajira ili kuharakisha maendeleo. Pia wameipongeza Serikali kwa mikakati waliyonayo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano kwa kuwa unaendana na vipaumbele vya Benki hiyo.
Benki hiyo imeitaka pia Tanzania kushiriki na kuchangamkia fursa za miradi ya kikanda hasa katika Nishati ya Umeme, Barabara na Reli na pia kuhakikisha utawala bora.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia)na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James (kushoto) wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), (hayupo pichani) alipokuwa akielezea umuhimu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wakati akizungumza na Wakurugenzi 12 wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki hiyo Mkutano uliofanyika jijini Dar es
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mpango (Mb) akizungumza na Wakurugenzi Watendaji 12 wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam.
Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza kwa Makini Maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini anayeiwakilisha nchi hiyo (AfDB) Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe (hayupo) pichani wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini anayeiwakilisha nchi hiyo (AfDB) Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe (kulia) akiipongeza Serikali kwa kuweka vipaumbele vya maendeleo vinavyoendana na vile vya Benki ya Maendeleo ya Afrika katika Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mpango (Mb) (kushoto) katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) akifafanua jambo wakati wa Mkutano wake na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini anayeiwakilisha nchi hiyo (AfDB) Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe (kulia) katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mpango (Mb), akiongoza mkutano ulio wakutanisha Wakurugenzi Watendaji wanaoziwakilisha nchi zao katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania huku ahadi zilizotolewa na Benki hiyo zikijadiliwa katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mpango (Mb), (katikati) na Kiongozi wa Ujumbe wa AfDB, Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe, kutoka Afrika Kusini (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wengine wanaowakilisha nchi zao katika Benki ya AfDB baada ya kumalizika kwa Mkutano katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mpango (Mb) (kulia) na Naibu wake Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kutoka Afrika ya Kusini anayeiwakilisha nchi hiyo (AfDB) Bi. Elizabeth Mmakgoshilekethe (katikati) wakibadilishana mawazo baada ya kumalizika kwa Mkutano kuhusu Hali ya uchumi nchini Tanzania katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es salaam.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM)
No comments:
Post a Comment