Na Benedict Liwenga-WHUSM
SERIKALI imesema kwamba tatizo la maradhi yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya akili yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku huku vyanzo vyake vikiwa ni pamoja na urithi, matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, matatizo ya kisaikolojia pamoja na hali ngumu ya maisha.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipokuwa akizindua Bodi ya Hospitali ya Mrembe Mkoani hapo.
Akiongea na mbele ya Watendaji wa Bodi hiyo, wageni waalikwa pamoja na Viongozi wa hospitalini hapo, Waziri Ummy amesema kuwa, kundi lililoathirika Zaidi na kdhai hiyo ni vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa, ambapo alitaja taarifa ya Shirikala Afya Ulimwenguni (WHO) ya mwaka 2016n inayoonyesha takribani watu milioni 15.3 Duniani wanapata matatizo ya kiafya yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na matumizi ya pombe kupita kiasi.
“Matatizo haya yamekuwa yakisababisha vifo milioni 3.3 kila mwaka Duniani kote, hata hivyo taarifa ya Wizata yangu inaonyesha kwamba idadi ya watu wanaougua magonjwa ya akili inaongezeka kwa kasi kubwa kutoka wagonjwa 136,710 mwaka 2011/2012 hado wagonjwa 448,997 mwaka 2015/2016”, alisema Ummy.
Ameongeza kuwa, takwimu za hospitali ya Mirembe zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka mine kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, jumla ya wagonjwa Zaidi ya 60,000 wenye magonjwa ya akili na waathirika wa dawa za kulevya walipatiwa huduma za afya na utengamao.
Aidha, kwa kutambua majukumu makubwa ya hospitali hiyo na kutatua changamoto zinazohusiana na magonjwa hayo, Serikali imeamua kuunda Bodi ya hospitalini hapo lengo likiwa ni kutekeleza dhana ya Utawala Bora na Utoaji wa Huduma Bora za Afya ya Akili kwa mujibu wa mapango mkakati na sera za nchi.
“Ninayo furaja leo kushiriki nanyi katika uzinduzi wa Bodi hii ya Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe, na bodi hii itaongozwa na Mwenyekiti pamoja na Wajumbe waliouteuliwa kutoka maeneo mbaimbali ya kiujuzi hapa nchini”, alisema Waziri Ummy.
Amesema kuwa, bodi hiyo itakuwa na majukumu mbalimbali yakiwemo kusimamia utendaji wa hospitali hiyo na Taasisi ya Isanga, kuhakikisha kuwa Sheria ya uanzishwaji wa hospitali inapatikana kwa wakati, kushauri kuhusu muundo wa hospitali, kuunda kamati ndogo ndogo, kushauri kuhusu mpango wa muda mrefu ili kuboresha huduma pamoja na kushauri jinsi ya kupunguza gharama za uendeshaji hospitalini hapo.
Sambamba na kuzindua bodi hiyo, Waziri Ummy ameitaka jamii kushirikiana na Serikali katika kupiga vita matumizi ya madawa ya kulevya hususan kwa vijana ili nguvu kazi ya Taifa isizidi kupotea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Gadi Kilonzo amempongeza Waziri Ummy na kwa kuzindua bodi hiyo na amemuhakikishia kuwa bodi hiyo itatekeleza maagizo yote pamoja na majukumu iliyopewa ili kuboresha utendaji kazi hospitakini hapo.
“Dhama uliyotupa sisi Wajumbe wa Bodi ni kubwa, tunaieheshimu sana na pia nakuahidi kuwa, tutatekeleza kwa bidii majukumu yote ya kuisimamia hospitali hii, tutajitahidi kwa uwezo wetu wote kutatua changamoto za hospitali hii kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya kupitia Wizara yako, pia tunashukuru kwa vifaa vya kazi ulivyotupatia kwa ajili ya kutumia wakati wa utendaji wetu”, alisem Kilonzo.
Wajumbe waliochaguliwa kuunda bodi hiyo ni Profesa Gadi Kilonzo ambaye ndio Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Erasmus Mndeme ambaye ni Katibu wa Bodi na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mirembe, Dkt. Mpona Boniventura ambaye ni Mwakilishi kutoka chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Joseph Mbatia, Ndugu John Sipendi, Ndugu Ernest Kabohola, Ndugu Jane Magembe pamoja na Ndugu Clavery Lyela.
No comments:
Post a Comment