Na Dennis Gondwe, IRINGA
Halmashauri ya
wilaya ya Iringa imetakiwa kusimamia sheria ya Mazingira vizuri ili kuondoa
uharibifu wa mazingira katika bonde la mto Ruaha mkuu.
Agizo hilo
lilitolewa na mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya mto
Ruaha mkuu ambaye pia ni Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu wakati
kikosi kazi hicho kilipokutana na timu ya menejimenti ya Halmashauri ya wilaya
ya Iringa jana.
Ayubu alisema
kuwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa
mazingira. “Ndugu zangu, sheria ya
Mazingira lazima isimamiwe ipasavyo. Katika kusimamia vizuri sheria hii wekeni
utaratibu mzuri wa kusimamia sheria hii kwa kuziimarisha kamati za mazingira
kuanzia ngazi za wilaya, kata na vijiji. Kamati hizi zikiimarishwa utekelezaji
wa sheria utakuwa mzuri na wenye kutoa matokeo mazuri zaidi” alisema Ayubu.
Aidha, alizitaka
kamati za Mazingira kutekeleza majukumu yake na kutoa taarifa za kazi kwa
mamlaka zinazohusika. Alisema kuwa utoaji wa taarifa utaziwezesha mamlaka kuwa
na picha kamili ya hali halisi ilivyo na kuwa na uelewa wa pamoja katika
kukabiliana na changamoto za kimazingira.
Ayubu aliitaka
Halmashauri hiyo kuelekeza miradi yote inayoanzishwa katika Halmashauri hiyo
kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa
vyanzo vya maji. Alisema kuwa ipo miradi ambayo imekuwa ikianzishwa pasipo
kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na kusababisha uharibifu wa
mazingira na vyanzo vya maji.
Aidha, aliitaka
Halmashauri hiyo kuweka mikakati imara ya kutekeleza uhifadhi wa mazingira. “Halmashauri ya wilaya ya Iringa lazima
muweke mikakati madhubuti inayotekeleza katika kusimamia uendelevu wa agenda ya
uhifadhi wa mazingira” alisema Ayubu.
Mwenyekiti huyo
alimtaka Mwanasheria wa Halmashauri kutoa elimu ya kina ya sheria ya Mazingira
na utekelezaji wake kwa kamati ya usalama ya wilaya ili kuiwezesha
inapotekeleza majukumu yake katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wa
afisa ardhi wa wilaya ya Iringa, Donald Mshani alisema kuwa Halmashauri ya
wilaya ya Iringa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira kutoka na
shughuli mbalimbali zikiwemo kilimo ndani ya mita 60 kutoka kingo za mito na
uingiaji wa mifugo mingi katika eneo ambalo halina uwezo wa kuihudumia. Alisema
kuwa katika kukabiliana na uharibifu huo, halmashauri ya wilaya ya iringa
imepanga kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote
vinavyozunguka eneo la bonde la mto Ruaha mkuu ili uhifadhi wa mazingira uweze
kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na kuwa endelevu.
Awali kaimu
mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Abel Mgimwa alizitaja
sababu zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika Halmashauri hiyo kuwa ni
ukataji miti ovyo kwa lengo la kuongeza ukubwa wa mashamba na uchomaji miti kwa
ajili ya mkaa. Sababu nyingine alizitaja kuwa ni wafugaji wengi kuingia maeneo
ya ukanda wa chini katika Tarafa za Pawaga na Idodi na wananchi kuanzisha
mashamba mapya jambo linalosababisha kuondolewa kwa uoto wa asili.
Mgimwa alisema
kuwa changamoto hizo suluhisho lake ni mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Aliongeza kuwa pamoja na mpango huo, sheria ndogo za vijiji kuhusu hifadhi ya
mazingira kwa vile vijiji ambavyo havina sheria hizo ili utekelezaji wake
uzingatiwe kikamilifu.
Halmashauri ya
wilaya ya Iringa ina jumla ya vijiji 133 kati ya vijiji hivyo, vijiji 61 ndivyo
vimefanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
No comments:
Post a Comment