Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Jakaya Kikwete amewahimiza Watumishi wa Umma kuendana na kasi ya maendeleo ya matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kwa pande zote za Muungano.
Ameyasema hayo jijini humo katika Kongamano la Pili la Utumishi wa Umma Tanzania 2026 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili nafasi ya utumishi wa umma katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 unahitaji utumishi wa umma wenye uwajibikaji, ufanisi, ubunifu na uwezo wa kusimamia kwa mafanikio sera na mipango ya Serikali ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga imani kwa Serikali yao.
“Dira ya Taifa 2050 kwa Tanzania Bara na Zanzibar zimeweka msingi wa kujenga taifa lenye uchumi imara, linalotumia maarifa, ubunifu na teknolojia katika kuleta maendeleo endelevu. Mafanikio ya utekelezaji wake yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa utumishi wa umma wa kisasa na wenye tija,” amesema Mhe. Kikwete.






No comments:
Post a Comment