HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

July 02, 2026

AZANIA BANK YAITIA CHACHU RIADHA DAR MASHINDANO YA TAIFA

NA MWANDISHI WETU 


TIMU ya Riadha ya Mkoa wa Dar es Salaam imeagwa rasmi kuelekea Mashindano ya Taifa ya Riadha yatakayorindima Julai 3-4 katika viwanja vya Shule za Filbert Bayi (FBS), Kibaha mkoani Pwani, huku ikitakiwa kuzingatia nidhamu na kujituma ili kurejea na ushindi.



Akizungumza wakati wa hafla ya kuikabidhi timu vifaa vya michezo vilivyodhaminiwa na Benki ya Azania, Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Kassim Semfuko, amesema nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio katika michezo na kuwataka wanariadha kuiwakilisha vyema Dar es Salaam.

"Tunawashukuru makocha kwa kuwaandaa vijana hawa licha ya muda mfupi wa maandalizi. Tuna imani mtakwenda kufanya vizuri na kurejea na ushindi," amesema Semfuko.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya Azania Tawi la Lumumba, Valentina Chasama., amesema benki hiyo itaendelea kuwa mshirika wa maendeleo ya riadha mkoani Dar es Salaam na kuahidi kuendelea kudhamini mashindano na shughuli mbalimbali za wanamichezo.

Amesema Benki ya Azania ina imani kubwa na uwezo wa wanariadha hao na kuwahimiza kujituma, kudumisha nidhamu na kupambana kwa ajili ya heshima ya mkoa.

"Tupo bega kwa bega na Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam na wanamichezo wote. Tunaamini mtauwakilisha vyema mkoa wetu na mtarejea na ushindi. Ushirikiano huu utaendelea hata katika mashindano mengine yajayo," amesema Chasama.

Amewataka vijana hao kutumia huduma za Benki ya Azania, ikiwemo akaunti maalumu za vijana, ili kuwawezesha kutimiza malengo yao ya michezo na maendeleo binafsi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam (DAA), Aman Ngoka, amesema timu hiyo imeandaliwa kupitia mashindano ya mkoa yaliyofanyika mapema mwaka huu na imejumuisha wanariadha wenye uwezo wa kuleta ushindani mkubwa.

Ngoka amesema mashindano hayo yanayoshirikisha mikoa 31 si ya kutafuta ubingwa pekee, bali pia ni jukwaa la wanariadha kufuzu kuiwakilisha Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola endapo watafikisha viwango vinavyohitajika.

"Tuna imani kubwa na vijana wetu. Tunaenda kufanya jambo kubwa kwa ajili ya Dar es Salaam na taifa kwa ujumla. Baadhi ya wanariadha wana nafasi ya kufuzu kuwakilisha Tanzania kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola iwapo watafikia viwango vinavyotakiwa," amesema Ngoka.



No comments:

Post a Comment

Pages