HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 05, 2017

Serikali ya Awamu ya Tano yapongezwa kwa Kuendelea kuimarisha Huduma za Afya

Frank Mvungi-Maelezo

Serikali  ya Awamu ya Tano imepongezwa kwa kuimarisha na kuendeleza miundo mbinu ya Afya,uboreshaji huduma kupitia teknolojia  na Usambazaji wa madawa  hadi kwenye vituo vya kutolea huduma.

Kauli hiyo imetolewa Leo Jijini Dar  es Salaam na Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bi Anna Makinda wakati akifungua Kongomano  la kwanza la bima ya afya na kinga ya jamii.

“’Lazima tuangalie na kuwatambua wale ambao hawawezi kulipia huduma za afya na tuangalie namna gani tutahakikisha wanapata huduma na isitokee wakati wowote wengine wakpoteza maisha kwa kukosa fedha za kujiunga na Bima ya Afya.’’ Alisisitiza Makinda.

Akifafanua Makinda amesema kuwa kuna umuhimu wa kuangalia namna huduma zinavyotolewa katika vituo vya kutolea huduma,upataikanaji wa vifaa tiba na dawa,hali inayochochea upatikanaji wa huduma bora kwakuwa ndiyo dhamira ya Serikali kupitia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Kuhusu Afya bora kwa wote Makinda alibainisha kuwa azma hiyo itafikiwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya na na mpango wa CHF iliyoboreshwa katika Halmashauri 50 hapa nchini.

Akizungumzia mkakati wa kutoa huduma bora Makinda amesema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umejipanga kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na watoa huduma zinaendana na dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma bora za afya.

Aliongeza kuwa watoa huduma watakao toa lugha zisizofaa kwa wagonjwa,kuwanyanyapaa, kuonyesha tabia ya ukatili watafungiwa kutoa huduma kama kituo hicho kimesajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Kwa Upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima nchini Dkt.Baghayo Saqware  amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwa na Sera ya Taifa ya Bima itakayowezesha wananchi huduma bora za Afya.

“Sera ya Taifa ya Bima tasaidiakuondoa tatizo la watoa huduma za Bima wasio waaminifu “ alisisitiza Dkt.Saqware.

Tanzania kama nchi imekuwa na historia ndefu ya kutoa huduma bora za matibabu kupitia bima ya Afya,Kuanzishwa kwa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF)Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Bima Binafsi zikiwa ni juhudi za kuboresha huduma hizo hapa nchini.

Kongamano la Bima ya Afya na Kinga limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) na shirika la Pharm Access International

No comments:

Post a Comment

Pages