HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 14, 2017

TADB, RIVACO WAJIPANGA KUWAWEZESHA WAKULIMA WA MAHINDI WA MANYARA


Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Manyara (RIVACO),  Lohay Langai (kushoto), akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Bodi ya RIVACO, kilichokuwa kinajadili namna ya kukiwezesha chama hicho kuweza kununua nafaka kutoka kwa wakulima wa mkoa wa Manyara. Kulia ni na Meneja wa Uendelezaji wa Biashara wa TADB,  Geofrey Mtawa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,  Francis Assenga. (Na Mpiga Picha Wetu).

Na Mwandishi wetu, Manyara

Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Manyara (Rift Valley Cooperative Union - RIVACO) wapo kwenye mazungumzo yatakayowezesha uhakika wa masoko kwa wakulima wa mahindi wa mkoani Manyara ili kuboresha usalama wa chakula nchini.
Katika kikao cha pamoja kati ya uongozi wa TADB na Bodi ya RIVACO pande hizo mbili zinajadiliana uwezekano wa kukiwezesha Chama hicho cha Ushirika kuweza kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa  mkoani Manyara.
Akizungumza wakati wa kikao hicho cha pamoja, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga anasema kuwa katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini, TADB ipo kwenye mpango wa kuikopesha RIVACO ili waweze kununua mahindi kutoka kwa wakulima mkoani humo.
“Kwa kuzingatia malengo ya kuanzishwa kwetu, TADB tuna madhumuni ya kuisaidia RIVACO ili kuhakikisha na kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake Bw. Lohay Langai ambaye ni Mwenyekiti wa RIVACO amesema Chama chake kinataka kutumia fursa za mikopo nafuu kutoka TADB ili waweze kutimiza lengo la Serikali la kuhakikisha chakula kinabaki nchini ili kuongeza usala wa chakula.
“Fursa za mikopo ya TADB inatupa nafasi ya kupewa mkopo kwa ajili ya kupata mtaji kwa ajili ya uendeshaji, uongezaji wa thamani na gharama za uhifadhi na masoko zitakazotuwezesha kununua mahindi kutoka kwa wakulima hali itakayochagiza usalama wa chakula nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha amesema kuwa kwa upande wa miundombinu ya masoko, TADB inatoa mikopo kwa minyororo ya thamani kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya masoko kama vile ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mahindi na miundombinu ya masoko na kugharamia usafirishaji  wa malighafi na unga ulio tayari kwenda sokoni.
“Pia Benki inagharamia uanzishaji wa mifumo ya upatikanaji wa taarifa za masoko pamoja na kuwezesha uhusiano wa masoko ya ndani na masoko ya kikanda na kugharamia mahitaji mengineyo ya kuwezesha miundombinu ya masoko,” alisema Bw. Chacha.
Kwa muda mrefu sasa ukosefu wa mtaji kwa vyama vya ushirika nchini kumesababisha wafanyabiashara kununua mazao mbalimbali na kuyauza nchi za nje hasa nchi za jirani hali inayosababisha usalama wa chakula nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages