HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 15, 2017

VYAMA VYA USHIRIKA VYA MSINGI MANYARA VYATEMBELEWA NA BENKI YA KILIMO

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akiwa na Mwenyekiti wa Homari AMCOS iliyopo katika Kijiji cha Masakta, Bibi Magreth Mgeni (kushoto) wakikagua mahindi katika moja ya mashamba waliyoyatembelea.

Na Mwandishi wetu, Manyara

Katika kufanikisha azma yake ya kuwa benki kiongozi  katika kuleta maendeleo ya kilimo nchini Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imevitembelea vya ushirika vya msingi mkoani Manyara ili kuangalia uwezekano wa kuwekeza mkoani humo.
Akizungumza wakati wa ziara zake katika vijiji vya Masakta, Gallapo na Gendi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema kuwa Benki yake ina Dira ya kuwa benki ya mfano na ya kisasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania kutoka kilimo cha kujikimu kwenda katika kilimo cha kibiashara na uzalishaji wenye tija katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Hivyo TADB ina wajibu wa kuwasaidia wakulima nchini ili kuwafikisha katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Bw. Assenga aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa kuwanyanyua wakulima katika uongezaji tija wa kilimo nchini kwa kutoa mikopo na kusaidia shughuli mbali mbali za uongezaji tija katika kilimo.
“Kwa kutambua umuhimu wa wakulima TADB kwa kushirikisha wadau wa Kilimo, utafiti na huduma za ugani tumejipanga kuwapatia wakulima mafunzo ya kilimo cha kisasa cha ili waweze kutumia mbinu bora za kilimo,” alisema.
Akizungumza katika kikao chao na ugeni wa TADB, Mwenyekiti wa Homari AMCOS iliyopo katika Kijiji cha Masakta, Bibi Magreth Mgeni alisema kuwa TADB imekuja wakati muafaka kwa kuwa itachagiza juhudi za kuinua na ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania.
“Kwa kweli tunapongeza kwa kuanzishwa Benki hii kwa kuwa kwa miaka mingi mikopo mingi kutoka taasisi za fedha imekuwa ikielekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa na kuwa na riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo,” alisema.
Naye Bw. Petro Dali, ambaye ni Mwenyekiti wa Gendi AMCOS alipongeza uanzishwaji wa TADB kwa kuwa licha ya umuhimu wa Sekta ya Kilimo, bado ukuaji wa sekta hiyo hasa kwa wakulima wadogo ulikuwa ukikabiliwa na changamoto mbali mbali kuu ikiwa ni ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini.
“Benki imekuja wakati muafaka kwa kuwa tunaamini itatusaidia katika kupata mikopo nafuu ya ununuzi wa pembejeo za kilimo na gharama na mahitaji mengine kwa ajili ya kuongeza tija katika kilimo,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Gallapo AMCOS, Bw. Orondi Doita alitoa wito kwa Benki ya Kilimo kuanza kuwakopesha ili waweze kujipanga mapema katika ununuzi wa mazao ili waweze kutimiza lengo la Serikali la kuhakikisha chakula kinabaki nchini ili kuongeza usalam wa chakula.
Kuanza kufanya kazi kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kunaleta suluhisho la changamoto nyingi zilizokuwa zinaikabili sekta kilimo nchini kwani inalenga kuboresha upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko.

No comments:

Post a Comment

Pages