Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kuwa itaendelea kuelimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mifumo,maudhui na taratibu za uridhiaji wa mikataba ili kufanya maandalizi stahiki kabla ya uridhiaji wa mikataba hiyo.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu Swali la Mhe.Ussi Pondeza Mbunge wa Chambani.
“Nchi yetu inazo sheria mbalimbali zinazotambua na kusimamia maslahi ya wafanyakazi nchini wakiwemo wafanyakazi wa majumbani,wafanyakazi wa mahotelini na vyama vyao”,Aliongeza Mhe,Mavunde.
Aidha Waziri Mavunde amewataka wafanyakazi nchini kutambua juhudi za Serikali za kulinda na kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi kupitia sheria,kanuni na taratibu zilizopo nchini.
Amesema Serikali inaendelea kupitia kwa makini azimio lililofikiwa na Shirika la kazi la Umoja wa Mataifa mwaka 2011 linaotaka kila nchi mwanachama wa ILO kuwa na Sheria ya kuwalinda wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani.
“Ni kweli kuwa Mwaka 2011,Nchi wanachama wa Shirika la Kazi Duniani ikiwemo Tanzania zilipitisha mkataba wa kimataifa kuhusu kazi za Staha kwa wafanyakazi wa Majumbani,ambapo hadi sasa nchi zilizoridhia ni 23 kati ya nchi 189 na kwa upande wa Afrika zimelizia nchi mbili tu kwa iyo bado tunaendelea kuupitia ili kufanya maandalizi ya kuridhia”,Aliongeza Mhe.Mavunde.
Pamoja na hayo Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Tanzania Bara ina sheria zake za kazi ambazo zinawahusu wafanyakazi wote ikiwemo wafanyakazi wa mahotelini na majumbani ambazo zinalinda haki zao.
No comments:
Post a Comment