WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la
upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini
ikiwemo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ilitengewa sh. bilioni 2.72 kwa
ajili ya ujenzi wa miradi ya maji.
Amesema
mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya
kumtua mama ndoo, wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya
maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi
yao.
Waziri
Mkuu aliyasema hayo jana (Jumapili, Julai 30, 2017) alipozungumza kwa
nyakati tofauti na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika
mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika wilaya ya
Rungwe, mkoani Mbeya.
Alisema
mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni 10.383 kwa ajili ya utekelezaji
miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake sh. bilioni 2.72
zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wilaya
ya Rungwe.
Waziri
Mkuu alitaja mradi mwingine unaotekelezwa wilayani Rungwe ni pamoja na
mradi wa maji wa Masoko wenye thamani ya sh. bilioni 5.3, utakaohudumia
jumla ya vijiji 15. “Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayojengwa chini
ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa fedha za ndani.”
Alisema mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika
vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi,
Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na
Nsanga.
Pia Waziri Mkuu alisema
wananchi lazima wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya
shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo
vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji kuwachukua hatua watu wote
watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa
makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa
zinasababisha ukame.
“Hatuwezi
kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu
mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji.
Ni marufuku
kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya
maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria.”
Awali
Mbunge wa Jimbo la Busokelo Mheshimiwa Fredy Mwakibete na mbunge wa
Rungwe Mheshimiwa Saul Amon walimueleza Waziri Mkuu kwamba upatikanaji
wa huduma ya maji na salama ni miongoni mwa changamoto zinazoyakabili
majimbo yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 31, 2017
No comments:
Post a Comment