*Ni baada ya kulisababishia Jiji
la Mbeya hasara ya sh. bilioni 63
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) mkoa wa Mbeya Bw. Emanuel Kiabo kumkamata na kumuhoji Mheshimiwa Atanas Kapunga aliyekuwa Meya
wa Jiji la Mbeya na wenzake 11 kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya sh.
bilioni 63.448.
"Serikali hii haiwezi ikawaacha
watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa halmashauri
moja. Kama wako humu ndani nagiza wakamatwe na waanze kuhojiwa na ambao wamestaafu
au kuhamishwa kituo cha kazi wasakwe popote walipo ili nao waje kuhojiwa.”
Waziri Mkuu ametoa
agizo hilo leo (Jumatatu, Julai 31, 2017) alipozungumza na watumishi wa Halmashauri
za wilaya
ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mkutano uliofanyika ukumbi wa
Benjamin Mkapa.
Wengine
ni waliowahi kuwa wakurugenzi wa Jiji hilo ambao ni Bw. Mussa Zungiza, Bi.
Elizabeth Munuo, Bw. Juma Idd na Dkt. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi
ya Ukurugenzi.
Aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji, Bw. James Jorojik pamoja na
waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ambao ni Bw. Mussa Mapunda, Bw. Samweli
Bubengwa, Bw. Davis Mbembela, Bi. Lydia Herbert na Bw. Bernard Nsolo ambao
walipitisha nyongeza ya mradi huo bila ya kuzingatia maslahi ya Jiji pamoja Emily
Maganga ambaye hakuishauri vizuri bodi hiyo.
Waziri Mkuu amesema watumishi hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kwa kuwa
wameisbabishia Serikali harasa kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko la
Mwanjelwa Jijini Mbeya ambalo hadi sasa
halijaonyesha tija.
Amesema mradi huo wa soko la Mwanjelwa uligubikwa na changamoto
nyingi kuanzia hatua za awali ambapo hata uchukuaji wa mkopo haukuwa
umezingatia mpango mkakati wa biashara, hivyo kusababisha Halmashauri ya Jiji
kuchukua mkopo zaidi ya kiasi kilichokusudiwa.
Waziri Mkuu amesema mbali na kuzidisha kiasi cha mkopo pia baada
ya kukamilika kwa ujenzi watuhumiwa hao waligushi mikataba ya upangaji, jambo
ambalo ni kinyume na matakwa ya Sheria
ya Manunuzi ya Umma. Pia waligawa vizimba kwa wafanyabiashara bila ya kupitia
mchakato wa manunuzi.
Amesema hata wahanga ambao walikuwepo awali kabla ya kuungua kwa
soko hawakupewa kipaumbele katika mchakato wa upangishaji wa soko jipya, ambapo
kwa hali ya kawaida ilitarajiwa wangekuwa wa kwanza kufikiriwa kutokana na
hasara waliyoipata baada ya kuunguliwa mali zao.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Bw. Amos
Makalla kukutana na Madiwani wa Halmashauri ya Jiji na kuweka mikakati na namna
gani wataweza kupanga bei ya vizimba katika soko hilo ili wafanyabiashara
wapange na wao kuweze kuanza kupata fedha za kupunguza deni.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
JULAI 31, 2017
No comments:
Post a Comment