Na Thobias Robert - MAELEZO
Tume
ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) itaendelea kusimamia kwa umakini ubora wa elimu
vyuo vikuu ili kuzalisha wasomi wenye tija kwa Taifa na kuongeza ufanisi,
ubunifu, maadili pamoja na utendaji kazi uliotukuka kwa vijana wanaohitimu
elimu ya vyuo vikuu nchini.
Hayo
yamesema leo na Afisa Habari Mwandamizi wa TCU Edward Mkaku wakati wa mahojiano
na mwandishi wa habari hii katika maonesho ya vyuo vikuu yanayoendelea katika Viwanja
vya Mnazi Mmoja Jijini, Dar es Salaam.
“Kwa
sasa TCU tunaratibu udahili ambao unafanywa na vyuo vikuu vyenyewe,
wakishamaliza kudahili majina yataletwa kwetu, na sisi tutapitia majina yote ili
kuyahakiki kama yana vigezo vyote vya kujiunga na chuo husika. Tutashirikiana na
Baraza la Mitihani na tukigundua kuna mtu amechomekewa kujiunga na chuo akiwa
hana vigezo tutamuondoa,” amefafanua Mkaku.
Amesema
kuwa tume hiyo itatembelea vyuo vyote nchini ili kufanya ukaguzi wa jina kwa
jina kwa ajili ya kujiridhisha, na kama ikitokea hakuna kasoro yoyote basi
mwanafunzi ataendelea na masomo.
Mkaku
aliongeza kuwa, ingawa zoezi la udahili limerudishwa vyuoni lakini bado TCU ina
mamlaka ya kusimamia ubora, mwenendo, mitaala pamoja na kozi zinazotolewa vyuoni
ili kukuza na kuendeleza elimu bora kwa ajili ya kuinua Taifa hasa wakati huu ambapo
Taifa linaelekea katika mapinduzi ya uchumi wa viwanda.
Aidha
amewataka wahitimu wawe makini katika kuzisoma kozi na kuchagua ili kusiwepo na
mkanganyiko na malalamiko yanayotokana na kukosea kuchagua au kupangiwa kozi
ambayo mhitimu hakuomba.
Hapo
nyuma zoezi la udahili wa vyuo vikuu lilikuwa likifanywa na TCU, lakini kutokana
na kuwepo kwa malalamiko mengi ya wanafunzi ya kupangiwa vyuo au kozi ambazo
hawakuzichagua ama kuzipenda, mapema mwaka huu Rais Dkt. John Pombe Magufuli
alisitisha zoezi la udahili kupitia TCU
na kuagiza udahili kufanyika moja kwa moja vyuoni kuanzia mwaka wa masomo wa
2017/18.
No comments:
Post a Comment