Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna mstaafu, Zelote Stephen, akizungumza kwenye baraza maalum la madiwani la kujadili na kujibu hoja 147 za mkaguzi wa hesabu za serikali nchini kwa mwaka wa fedha 2015-16 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. (Na Mpiga Picha Wetu).
RUKWA, TANZANIA
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wale wote watakaosababisha kuibuka kwa hoja za ukaguzi wa Hesabu za serikali katika Halmashauri zao.
RUKWA, TANZANIA
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wale wote watakaosababisha kuibuka kwa hoja za ukaguzi wa Hesabu za serikali katika Halmashauri zao.
aliyasema hayo alipohudhuria kwenye baraza maalum la madiwani la kujadili na kujibu hoja 147 za mkaguzi wa hesabu za serikali nchini kwa mwaka wa fedha 2015/2016 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Akinukuu barua ya maagizo aliyoyatoa tarehe 4/5/2017 Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kila mamlaka ya nidhamu ichukue hatua za kinidhanmu kwa mujibu wa sharia kwa watumishi ambao wamesababisha hoja za ukaguzi kwa uzembe au kwa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na taarifa juu ya hatua hizo apelekewe.
“Kwenye hoja zilizojibiwa ningependa sana hoja ziwe na data zinazoeleweka na za uhakika, na kuacha kitu kinachoitwa tunaendelea kuishughuilikia, iseme tumefikia wapi, sio tunaendelea, Hakuna kinachoendelea, lazima kupiga hatua kuondoka kwenye hoja hiyo, nimesikia kuwa kuna watu wamechukuliwa hatua lakini sijaziona,” Mh. Zelote alibainisha.
Aidha alibainisha kuwa wapo watu waliofanya madudu na wanapaswa kuchukuliwa hatua na kutowaachia kwani kufanya hivyo hakutasaidia kufutika kwa hoja na kusisitiza kuwa waliosababisha hoja watafutwe popote walipo ili warudi kujibu hoja walizoziibua.
Hata hivyo, Mh. Zelote ameusifu uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa kuweka misingi imara iliyowapelekea kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na kuwaasa kumtumia mkaguzi mkaazi wa mkoa pamoja na wakaguzi wa ndani kutoka ofisi yake ili kuzuia hoja zisitokee.
“Ni halmashauri pekee katika Mkoa huu ambayo imepata hati safi, kwa hilo niwapongeze sana, angalau mmenitoa kimasomaso, sijui ingekuwaje kama ingekuwa ni zote zimepata hati yenye mashaka,” Alisema.
Na kuagiza kuwa hoja zote zilizo ndani ya uwezo wa mkoa zisijitokeze tena kwakuwa halmashauri zote zina mfumo unaojumuisha kanuni, sharia na taratibu lazima mambo hayo yasimamiwe kikamilifu.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mh. Zeno Mwanakulya alisema kuwa lengo la halmashauri ni kuhakikisha kuwa hoja hizo zinafutika na hazijirudii.
“Lengo la Halmashauri ni kuhakikisha kwamba tunazifuta hoja zote, ndio lengo letu kubwa kwahiyo wakati tunachangia lazima tujiulize kwanini hoja hizi zimejitokeza, Je, zilikuwa na sababu ya kutokea, basi ni vizuri kama wawakilishi wa wananchi tuweke msisitizo hoja hizo zifutwe” Alisema.
Na pia aliahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kupata hati safi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alibainisha kuwa hoja zinasababishwa na uzembe wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao na kukumbusha kuwa mwaka wa fedha 2014/2015 kulikuwa na hoja 80 ukilinganisha na mwaka wa fedha 2015/2016 wenye hoja 147.
“Kila mtu katika eneo lake akiwajibika hakutakuwa na hoja kwasababu Hakuna hoja isiyo na majibu, wakaguzi wanachotaka ni majibu, ukishawaridhisha kwa kuweka kumbukumbu zako vizuri, hoja haiwezi kujitokeza,” alimalizia.
No comments:
Post a Comment