Kocha Mkuu wa timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’,
Salum Mayanga (pichani) amemwongeza Kiugo wa Young Africans, Emmanuel Martin
kwenye kikosi chake kinachojindaa kucheza na Botswana Jumamosi Septemba
2, mwaka huu.
Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kwenye Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam chini ya utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Emmanuel Martin anatarajiwa kujiunga na kambi ya Taifa Stars mara
moja leo Agosti 30, mwaka huu na kuanza na mazoezi na wenzake
yatakayofanyika jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Emmanuel Martin ameongezwa na Mayanga baada ya mawasiliano kuonesha
kwamba huenda akawakosa nyota wa kimataifa Simon Msuva kutoka Difaa El
Jadidah ya Morocco na Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno.
Taarifa kutoka Morocco inaonesha kwamba Msuva ana kibali cha muda cha
kuingia na kutoka Morocco ‘visa’ ambacho kinamnyima haki ya kutoka na
kuingia Morocco mara kwa mara.
Kuna juhudi zinafanywa na timu yake kadhalika Shirikisho la Mpira wa
Miguu la Morocco kumfanikishia kupata kibali cha muda mrefu ili iwe
rahisi kwa mchezaji kutoka na kuingia kama anahitaji katika timu ya
taifa.
Kuhusu Mollel taratibu za ruhusa za kimataifa zinafanyiwa kazi kwa
mujibu wa sheria za nchi ya Ureno ambako anacheza soka la kulipwa.
Nyota wengine wote wameripoti Taifa Stars wakiwamo wale wa kutoka nje
ya mipaka ya Tanzania kama vile Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji),
Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini),
Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya) wakati Farid Mussa wa CD Tenerif ya
Hispania anatarajiwa kutua leo.
Wengine ambao wako kambini Hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar
es Salaam ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na
Ramadhani Kabwili (Young Africans).
Pia wamo Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga
(Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na
Erasto Nyoni (Simba SC).
Viungo ni Himid Mao - Nahodha Msaidizi (Azam FC), Mzamiru Yassin
(Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza Kichuya (Simba SC), wakati
Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans) na Kelvin Sabato (Azam
FC).
Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni
Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha
wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu),
Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
No comments:
Post a Comment