HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 12, 2017

WADAI JNIA KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA ENDAPO HAWAJALIPA MADENI YAO HADI SEPTEMBA 30

Mhe. Prof. Makame Mbarawa (aliyeshika simu mbele katikati) akielekea katika jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kukagua maeneo mbalimbali mara baada ya kumalizikakwa mkutano wa wadau wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye jengo hilo, aliouitisha kuwasisitizia wanaodaiwa walipe kodi kabla ya Septemba mwaka huu. Mwenye suti mbele ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi akimkaribisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa kuongea na wafanyabiashara wa ndani na nje ya jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Watu Mashuhuri (VIP).
Meneja wa Kituo wa ndege ya Shirika la ndege la Oman, Bw. I shaqar (aliyesimama) akimweleza Mhe. Prof Makame Mbarawa mambo mbalimbali, kwenye mkutano wa wadau wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye  Jengo la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) leo, ambapo Mhe. Mbarawa ameagiza wadau wote wanaodaiwa kodi walipe haraka na mwisho ni Septemba mwaka huu.
Mhe.Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (aliyeshika diary) wakati akikagua moja ya mashine za kukagua mizigo ya abiria, baada ya kumaliza mkutano aliouitisha wa wadau wanaofanya shughuli mbalimbali JNIA. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Salim Msangi.  
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Bw. Hamza Johari akizungumza na wadau wanaofanya shughuli mbalimbali  kwenye  Jengo la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) leo, katika mkutano ulioitishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Precision, Bi. Sauda Rajabu akitoa hoja mbalimbali kwenye mkutano wa wadau wanaofanya shughuli zao kwenye jengo la abiria la Kiwanja cha Ncdege cha Kimataifa cha Julius Nyerere,ulioitishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa leo.
Wadau mbalimbali wanaofanya shughuli kwenye jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere wakimsikiliza Mhe. Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) katika mkutano ulioitishwa leo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo ya ulipaji wa kodi. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Watu Mashuhuri (VIP).
 Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amewapa hadi tarehe 30 mwezi Septemba mwaka huu 2017 wadau wote wanaoendesha shughuli zao mbalimbali kwenye Jengo la abiria la Pili la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Mhe. Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo leo alipokutana na wadau hao kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Watu Mashuhuri (VIP-TBII), kwa lengo la kujua changamoto wanazokutana nazo na kujadili namna ya kuzitatua.
Amesema wadau hao ni wengi ila baadhi yao ni wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali zilizopo kwenye maduka, mashirika ya ndege, watoa huduma za vyakula, vinywaji, mitandao ya simu, huduma za usafiri na huduma za kifedha, lakini wamekuwa wakifanya shughuli zao bila ya kulipa kodi kwa muda mrefu, jambo ambalo linaloisababishia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kushindwa kutoa huduma bora.
“Serikali inafanya biasharana wao wanafanya biashara lazima kufanikiwa kwa biashara hii tuwe na hali ya kuelewana, sisi tuweze kupata na wao vilevile, na tumewaambia wengi wao wamekuwa hawalipi kodi kwa muda mrefu na sasa wakati umefika kila mtu alipe kodi, na serikali kupitia TAA itaweza kutoa huduma za kuridhisha,” amesema Mhe. Prof. Mbarawa.

Hatahivyo, amesema kwa muda Mfupi wameweza kukusanya mapato ya kiasi cha shilingi bilioni 6.7,  pamoja na bado wengi wao wanadaiwa kodi.
Pia Mhe. Prof. Mbarawa amesema sasa watakwenda na wakati kwa kuangalia soko la maeneo ya biashara kwenye viwanja vya ndege na kutoza kulingana na mwelekeo wa soko hilo, ambapo sasa wadau hao wamekuwa wakitozwa kodi bila kuangalia muda aliopangisha ambapo wengine wanazaidi ya miaka 10, lakini bado wanalipa kodi ya mwaka walioingilia.
“Hawa ni wateja wangu na tumeingia mikataba nao hivyo siwezi kusema kuwa wanadaiwa kiasi gani, ila wamekuwa wakishindwa kulipa kodi kwa wakati matokeo yake baadhi ya huduma zinashindwa kufanyika kwani mamlaka inakuwa inashindwa kwa kuwa haina fedha, hivyo nimewapa hadi tarehe 30 na atakayeshindwa ajiondokee,” amesisitiza Mhe. Mbarawa.
Akizungumzia msongamano katika eneo la ulipaji wa visa kwa abiria wanaotoka nje ya nchi, amesema tayari kumekuwa na mazungumzo na mashirika ya ndege ili kuona utaratibu wa kurekebisha ratiba zao za kuwasili kwa kupishana saa mbili tofauti na sasa zinapishana muda mfupi na zinakuwa na abiria wengi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi amesema wanaimani wadaiwa wote watalipa madeni yao kama walivyopewa muda wa mwisho na Mhe. Waziri.
“Ila kuna wale ambao tumewapeleka mahakamani sasa tunasubiri taratibu za kimahakama zimalizike, lakini pia kuna wale ambao walishafunga ofisi siku nyingi na hatuna uhakika wa kuwapata tena na tunaanzisha utaratibu wa wa kuiomba serikali ili madeni yao yafutwe kabisa,” amesema Bw. Msangi.

No comments:

Post a Comment

Pages