WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
imeamua kufufua mazao matano ambayo yanaingiza kwa wingi fedha za kigeni
nchini.
Amesema mbali ya korosho, Serikali imeamua
kuboresha mazao ya tumbaku, chai, kahawa na pamba.
Ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana na leo wakati
akiwahutubia wananchi kwenye maeneo mbalimbali akiwa katika ziara ya kikazi ya
siku nne mkoani Tabora.
Alisema kuanzania sasa serikali imepiga marufuku
matumizi ya dola za Marekani kwenye ununuzi wa zao la tumbaku kwa sababu mazao
mengine makuu hapa nchini yananunuliwa kwa fedha za Kitanzania.
“Ni kwa nini tumbaku inunuliwe kwa dola za Marekani
ilhali mazao mengine yananunuliwa kwa fedha za Tanzania? Korosho, pamba, chai
na kahawa wakulima wetu kote huko wanalipwa kwa fedha za Tanzania, kwa nini
tumbaku iwe tofauti?” alihoji.
Alisema wenye makampuni wanaweza kukaa kwenye vikao
vyao na kupanga bei zao kwa dola za Marekani lakini pindi wanapoingia nchini,
watalazimika kufanya malipo kwa kutumia fedha ya Tanzania kwani mfumo malipo
kupitia dola za Marekani umekuwa ukiwaibia wakulima kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu amewataka watendaji na watumishi wa
Halmashauri na wilaya za mkoa wa Tabora wasimamie zao la tumbaku ili kuinua
kilimo cha zao hilo na kuwanufaisha wakulima.
"Maafisa kilimo na maafisa ushirika mnapaswa
kulisimamia zao hili na siyo kuwaachia maafisa wa makampuni yanayonunua
tumbaku."
“Kwa muda mrefu mlizembea na kuwaachia maafisa wa
makampuni ya ununuzi ndiyo washughulike na wakulima. Nataka mbadilike, kuweni
karibu na wakulima na muwasaidie kulima kisasa na kwa kutumia pembejeo,"
alisema.
"Wasaidieni wakulima watoke kwenye mfumo wa
kukopa pembejeo, wahimizeni wajiwekee akiba ili msimu ukianza wawe na fedha ya
kununua pembejeo. Wakulima wanalaliwa sababu ya mikopo ya pembejeo. Makato
yanakuwa mengi kiasi kwamba mkulima ahambulii chochote," alisema.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani
Kaliua ambako atazungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 11, 2017.
No comments:
Post a Comment